UFARANSA-JAMUHURI YA AFRIKA YA KATI

Majeshi ya kulinda amani yafanya Oparesheni ya kupokonya silaha makundi ya wapiganaji mjini Bangui

Jeshi la kulinda amani nchini Jamhuri ya Afrika ya kati limefanikiwa kukamata silaha lukuki mjini humo
Jeshi la kulinda amani nchini Jamhuri ya Afrika ya kati limefanikiwa kukamata silaha lukuki mjini humo REUTERS/Luc Gnago

Nchini Jamuhuri ya Afrika ya kati Majeshi ya kulinda amani kutoka Ufaransa na umoja wa Afrika yamefanikiwa kupokonya silaha kutoka mikononi mwa makundi ya wapiganaji katika mji wa Bangui licha ya kushindwa kuwatia nguvuni viongozi wa makundi yanayoendesha mapigano.

Matangazo ya kibiashara

Ukaguzi wa nyumba kwa nyumba ukifanywa na wanajeshi takribani mia mbili na hamsini Ulidumu kwa takribani masaa manne mjini Bangui ambako wapiganaji wa kristo wamekita kambi na kufanya mashambulizi dhidi ya waislamu hivi karibuni.

Mwa mujibu wa shirika la habari la ufaransa AFP Silaha mbalimbali zimepatikana katika zoezi hilo ikiwemo mabomu ya viwandani na ya kutengenezwa kienyeji.

Mwishoni mwa juma Ufaransa iliarifu mpango wa kuongeza wanajeshi mia nne zaidi ili kuimarisha oparesheni za kiusalama nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati ambapo Rais Francois Hollande alisema Paris inaongeza idadi hiyo ili kufikisha wanajeshi 2000 nchini humo.

Rais Hollande pia aliutaka Umoja wa Ulaya EU kuharakisha mpango wa upelekaji wa wanajeshi wake 500 huku akiahidi kuwa serikali yake itaendeleza jitihada za kukomesha mauaji, unyanyasaji na kurejesha usalama.

Wanadiplomasia wa Ulaya wanasema majeshi hayo yataanza kuingia mjini Bangui mwezi ujao, baada ya mapema juma hili Mawaziri wa EU kuipa oparesheni hiyo muda wa miezi tisa.