THAILAND-Sheria

Waziri mkuu wa Thailand akabiliwa na mashataka ya ubadhrifu

Waziri mkuu wa Thailand, Yingluck Shinawatra
Waziri mkuu wa Thailand, Yingluck Shinawatra RFI

Waziri mkuu wa Thailand anakabiliwa na mashtaka ya kushindwa kutekeleza majukumu yake kama kiongozi, wakati huu polisi wakikabiliana na waandamanaji wanaoipinga Serikali mjini Bangkok. Tangazo hili limetolewa na tume ya kupambana na rushwa nchini humo ambapo tume hiyo inadai kuwa waziri mkuu Yingluck Shinawatra alifanya uzembe wakati wa utoaji wa zabuni ya ununuzi wa pembejeo za kilimo cha mpunga.

Matangazo ya kibiashara

Iwapo atapatikana na hatia ya makosa yanayomkabili, huenda akapoteza nafasi yake kama waziri mkuu.

Watu 4 wamepoteza maisha na wengine zaidi ya 60 wamejeruhiwa kufuatia maandamano ya vurugu kati ya polisi na wananchi wanaopinga serikali.

Hayo ni baada ya viongozi nchini Thailand kuamuru polisi kuanzisha jana jumanne operesheni kabambe ili waweze kurejesha kwenye himaya ya serikali maeneo mengi ambayo yameshikiliwa na waandamanaji kwa miezi kadhaa sasa. Askari polisi mmoja ameuawa.

Waziri mkuu Yingluck Shinawatra alizungumza kupitia televisheni msimamo wa serikali.

Waandamanaji katika moja ya maeneo ya kaskazini ya mji wa Bangkok wanaoongozwa na mmoja wa viongozi wa madhehebu ya kibudisti Luang Pu Buddha Issara, walikubali, baada ya mazungumzo, kuondoka katika eneo walilokua wakishikilia tangu mwanzoni mwa mwezi wa januari.

Hali ya sintofahamu ilipotiwa mapema jana asubuhi kwenye makao makuu ya serikali katika eneo la kihistoria la Bangkok.

Askari polisi wa kuzima fujo walivurumisha mabomu ya kutoa machozi na kufyatua risasi za plastiki ili kujaribu kutawanya kundi moja la waandamanaji lenye msimamo mkali lilokua limeweka barabarani vizuizi vya mifuko ya mchanga na vyuma.