DRC: Monusco inajianda kutuma kikosi cha wanajeshi wake katika jimbo la Katanga

mkuu wa majeshi ya Umoja wa Mataifa nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (Monusco) Carlos Alberto dos Santos Cruz
mkuu wa majeshi ya Umoja wa Mataifa nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (Monusco) Carlos Alberto dos Santos Cruz Sylvain Liechti/MONUSCO

Tume ya Umoja wa mataifa nchini Jamhuri ya kidemokrasia ya kongo Monusco, imesema kuwa itawatuma wanajeshi wake ili kulinda raia katika mji wa Pweto Jimboni Katanga eneo ambalo limekuwa likishuhudia mapigano ya mara kwa mara kati ya jeshi la serikali FARDC na wapiganaji wa kundi la Bakata katanga.

Matangazo ya kibiashara

Jambo la Katanga linapatikana kusini mashariki mwa jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.

Akizungumza Kwenye mkutano na wanahabari mjini Kinshasa kamanda mkuu wa Jeshi la umoja wa mataifa nchini Congo, Jenarali Carlos Santos Cruz amesema kuwa baada ya kuitathmini hali ya usalama katika eneo hilo, wameona kuwa ni Muda wa kuchukua  hatua ya kuhakikisha Usalama unazingatiwa katika eneo hili, lililofahamika kama Bonde la mauti, katika Jimbo hilo la Katanga.

“Tutawatuma hivi karibuni wanajeshi wa kikosi cha Umoja wa Mataifa katika mji wa Pweto”, mji unaopatikana katikati mashariki mwa jimbo la Katanga ambalo lina ukubwa sawa na taifa la Uhispania, amesema mkuu wa majeshi ya Umoja wa Mataifa nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (Monusco) Carlos Alberto dos Santos Cruz, katika mkutano na waandishi wa habari.

Amebaini kwamba watatuma wanajeshi waliyo kati ya 100 na 120 katika mji wa Pweto.

Afisa huyo wa jeshi kutoka Brazil, amesema idadi ya wanajeshi 450 wanaopatikana katika jimbo la Katanga ni ndogo, ikilinganishwa na ukubwa wa jimbo hilo.

Miji ya pweto, Mitwaba na Manono imetajwa kuwa sehemu hatari, ambako wapiganaji wa kundi la Mayi mayi Bakata Katanga wameendelea na mapigano huku wakidai kwamba watahakikisha Jimbo la Katanga linapata uhuru wake.

Kwa mujibu wa ofisi ya Umoja wa Mataifa ya kuratibu masuala ya kibinadamu (OCHA), watu 400,000 wameyahama makaazi yao, huku 60,000 miongoni mwao wakiwa ni kutoka katika mji wa Pweto.