Waziri mkuu wa Thailand akanusha tuhuma za ubadhirifu zinazomkabili
Waziri mkuu wa Thailand, Yingluck Shinawatra amejitokeza kwa mara ya kwanza na kujitetea dhidi ya tuhuma zinazomkabili za matumizi mabaya ya ofisi na kushindwa kuwajibika kama kiongozi. Utetezi wa Yingluck unakuja wakati huu ambapo tume ya kupambana na rushwa nchini humo ikiwa imewasilisha kesi mahakamani, kumshtaki waziri mkuu huyo kwa kushindwa kuwajibika na kuisababishia nchi hasara ya mamilioni ya fedha kutokana na pembejeo za kilimo cha mpunga.
Imechapishwa:
Kiongozi huyo amekana tuhuma hizo akisisitiza ni njama za kutaka kumn'goa madarakani wakati huu ambapo waandamanji wakiendelea kukaidi tangazo la jeshi kuwataka waondoke kwenye maeneo wanayoyakalia.
Hayo yanajiri wakati maelfu ya wakulima wa mchele wamefahamisha leo ijumaa kwamba wataandamana wakielekea kwenye uwanja wa ndege wa mjini Bangkok, wakimuonya rais Yingluck Shinawatra, kutekeleza madai yao ya kulipwa deni la mchele waliyoitolea serikali.
Wakulima hao wametishia kuandamana hadi kwenye uwanja wa ndege wa Suvarnabhumi, lakini wamesitisha maandamano hayo kaskazini mwa mji mkuu, na wamekubali kurejea makwao, baada ya kuafikiana na serikali, ambapo kulingana na taarifa ziliyotolewa na vyombo vya habari, serikali huenda imeahidi kuwalipa juma lijalo.
Awali majaji katika mahakama kuu nchini Thailand ilionya Polisi nchini humo kuwaomba kwamba wasitumie nguvu kupita kiasi kuvunja maandamano ya amani, wakati huu waandamanaji mjini Bangkok wakisisitiza kuongeza shinikizo kumng'oa madarakani waziri mkuu Yingluck Shinawatra.
Tangazo hilo la mahakama lilitolewa wakati nchi hiyo ishuhudia juzi jumanne makabiliano mabaya zaidi kati ya polisi na waandamanaji ambapo watu watano walipoteza maisha na wengine kadhaa kujeruhiwa.
Mpaka sasa zaidi ya watu kumi na sita wamepoteza maisha kwa pande zote mbili toka kuanza kwa maandamano hayo miezi mitatu iliyopita ambapo hivi karibuni watu wengi wamekuwa wakijeruhiwa kutokana na risasi na mabomu ambapo kila upande unamtuhumu mwenzake kutumia silaha za hatari.
Hayo ni baada ya viongozi nchini Thailand kuamuru polisi kuanzisha juzi jumanne operesheni kabambe ili waweze kurejesha kwenye himaya ya serikali maeneo mengi ambayo yameshikiliwa na waandamanaji kwa miezi kadhaa sasa.