UKRAINE-Siasa

Oleksandre Turchinov ateuliwa kuwa rais mpya wa mpito wa Ukraine

Rais mpya wa mpito wa Ukraine, Oleksandre Tourtchinov (kushoto), akiwa na Ioulia Timochenko, waziri mkuu wa zamani (kulia), januari 13 mwaka 2009, wakiwa katika jengo la bunge mjini Kiev.
Rais mpya wa mpito wa Ukraine, Oleksandre Tourtchinov (kushoto), akiwa na Ioulia Timochenko, waziri mkuu wa zamani (kulia), januari 13 mwaka 2009, wakiwa katika jengo la bunge mjini Kiev. AFP/Genia Savilov

Hatimae nchi ya Ukraine imempata rais mpya baada ya maandamano na ghasia kujitokeza nchini humo kwa takriban miezi mitatu na kusababisha aliyekuwa rais wa nchi hiyo Voctor Ianukovich kuikimbia nchi yake. Mgogoro huo wa kisiasa umefikia kilele chake mwishoni mwa juma lililopita ukigubikwa na mapigano ya kikatili yaliyosababisha mauwaji ya zaidi ya watu 82 ndani ya siku tatu.

Matangazo ya kibiashara

Bunge nchini humo, likiwa na wapinzani wengi ambao waliongoza mapambano hayo, limemteuwa Oleksandre Turchinov, ambae ni mshirika wa karibu wa mpinzani wa utawala wa Viktor Ianoukovitch, Ioulia Timochenko, huku baraza la mpito la mawaziri likisubiriwa kuundwa siku za usoni.

Bunge la Ukraine linatarajiwa kukutana leo kwa minajili ya kuunda serikali mpya ya mpito, baada ya taifa hilo kushuhudiwa machafuko yaliyodumu miezi mitatu.

Mkuu wa sera za nje wa Umoja wa Ulaya, Catherine Ashton, anasubiriwa leo mjini Kiev kujadili hatua zitakazochukuliwa ili hali ya usalama irejeye nchini na kuweka sawa sekta ya uchumi ambayo inaendelea kudorora nchini humo, wakati mataifa ya magharibi yalizidisha wito jana wa kuheshimu uhuru wa taifa na kukinga ili Ukraine isikumbwi na hali ya mgawanyiko.

Wakati hayo yakijiri, Rais wa Urusi Vladmiri Putin amemwitisha balozi wake nchini Ukraine kwa mashauriano zaidi, huku viongozi wa Ulaya na Marekani wakipongeza hatua iliyofikiwa na kuomba machafuko yasitishwe mara moja kusubiria uchaguzi wa rais utakaofanyika tarehe 25 mwezi Mei mwaka huu.

Waziri wa mambo ya nje wa Ufaransa, Laurent Fabius, amepongeza hatua hio, na kubaini kwamba bara la Ulaya liko tayari kuisaidia serikali ya mpito.

“Hali nchini Ukraine imekuwa mpya, rais Yanukovich tayari ameondoka, na katika muktadha huo, msimamo wa Ulaya hususan wa Ufaransa ni kuisaidia serikali hii ya mpito na ya kidemokrasia, kuwatakia amani na umoja wa kitaifa uheshimiwe.Sasa kuna chama tawala kipya, na lazima uhuru na umoja wa kitaifa viheshimiwe na demokrasia hii ya mpito ifikie malengo yake”, amesema Laurent Fabius.

Wachambuzi wa masuala ya kisiasa wanazungumzia hatua hiyo kuwa matokeo ya msimamo wa bunge nchini humo ambalo kwa muda mrefu halikutaka kumuunga rais mkono.