SUDAN-MAzungumzo

Mazungumzo ya kusitisha mapigano nchini Sudan yanatazamiwa kuanza

Thabo Mbeki (kushoto) na rais Omar al-Bashir (kulia), mjini Khartoum, nchini Sudan, mei 22 mwaka 2012
Thabo Mbeki (kushoto) na rais Omar al-Bashir (kulia), mjini Khartoum, nchini Sudan, mei 22 mwaka 2012 AFP/Ebrahim Hamid

Mpatanishi mkuu wa Umoja wa Afrika kwenye mzozo wa Sudan, rais wa zamani wa Afrika kusini, Thabo Mbeki amewasili mjini Khartoum ambako amekuwa na mazungumzo na viongozi wa Serikali kabla ya kuanza mazungumzo na waasi wa jimbo la Kordofan Kusini.

Matangazo ya kibiashara

Thabo Mbeki amewasili nchini Sudan ikiwa zimebaki siku tatu tu kabla ya kuanza kwa mazungumzo ya amani kati ya serikali ya Khartoum na waasi wa Kordofan Kusini, mazungumzo yanayotarajiwa kuanza Ijumaa ya wiki hii.

Kuanza kwa mazungumzo haya kumekuwa kama hatua ya kushtukiza kwa kuwa pande zote mbili zilisisitiza kutoketi kwenye meza ya mazungumzo kujaribu kumaliza mzozo wa Jimbo hilo na lile la Blue.

Mara baada ya ziara yake nchini Sudan, Thabo Mbeki ataelekea mjini Addis-Ababa, Ethiopia tayari kwa maandalizi ya mazungumzo hayo.

Tayari serikali ya Sudan na waasi wa jimbo la Kordofan Kusini wanajadili pendekezo la kusitisha mapigano, liliyotolewa na wasuluhishi wa Umoja wa Afrika, ili kuyapa nafasi mashirika ya kutoa misaada kuwahudumia raia zaidi ya milioni moja.

Wasuluhishi wametoa pendekezo hilo jana jumanne, huku wakiitaka serikali ya Khartoum na waasi kuliheshimu. Pande hizo mbili zimekua zikilaumiana kila mmoja kukwamisha mazungumzo.

Mazungumzo kati ya Khartoum na waasi yanalenga kusitisha kwa mapigano, ambayo yamedumu kwa miaka mitatu sasa katika majimbo ya Kordofan na Nil, machafuko ambayo yamewagusa raia zaidi ya milioni moja.

Hadi sasa haijajulikana idadi ya watu waliyopoteza maisha katika majimbo ya Kordofan na Nil. Kwa mujibu wa Umoja wa mataifa, watu milioni 1.2 wameguswa na machafuko hayo au walilazimika kuyahama makaazi yao.