SUDAN-SUDAN KUSINI-Mazungumzo

Umoja wa Afrika utahakikisha tofauti za kimipaka kati ya serikali ya Sudan na Sudan Kusini zinapatiwa ufumbuzi

Umoja wa Afrika umesema kuwa juma hili unatarajia kusimamia mazungumzo mapya kati ya waasi wa Sudan na Serikali ya Khartoum, mazungumzo yanayolenga kujaribu kumaliza tofauti za kimipaka kati yake na Sudan Kusini.  

Mpatanishi mkuu wa Umoja wa Afrika katika mgogoro wa mipaka kati ya Sudan mbili na rais wa zamani wa Afrika Kusini, Thabo Mbeki
Mpatanishi mkuu wa Umoja wa Afrika katika mgogoro wa mipaka kati ya Sudan mbili na rais wa zamani wa Afrika Kusini, Thabo Mbeki AFP
Matangazo ya kibiashara

Mara baada ya mazungumzo yake na rais Omara Hassan Al-Bashir, mpatanishi mkuu wa Umoja wa Afrika na rais wa zamani wa Afrika Kusini, Thabo Mbeki, amewaambia wanahabari mjini Khartoum kuwa wamekubaliana na rais Bashir kuwa na mazungumzo na waasi mwishoni mwa juma hili mjini Addis Ababa, Ethiopia.

Hili ni jaribio la pili la Umoja wa Afrika kutaka kuikutanisha serikali ya Khartoum na waasi wa SPLM-N, ambapo mazungumzo ya awali yaligonga mwamba tarehe 18 ya mwezi huu mjini Addis-Ababa bila ujumbe wa pande zote mbili kukutana ana kwa ana.

Thabo Mbeki aliwasili nchini Sudan ikiwa zimebaki siku mbili tu kabla ya kuanza kwa mazungumzo ya amani kati ya serikali ya Khartoum na waasi wa Kordofan Kusini, mazungumzo yanayotarajiwa kuanza Ijumaa ya wiki hii.

Kuanza kwa mazungumzo haya kumekuwa kama hatua ya kushtukiza kwa kuwa pande zote mbili zilisisitiza kutoketi kwenye meza ya mazungumzo kujaribu kumaliza mzozo wa Jimbo hilo na lile la Blue.

Mara baada ya ziara yake nchini Sudan, Thabo Mbeki ataelekea mjini Addis-Ababa, Ethiopia tayari kwa maandalizi ya mazungumzo hayo.

Tayari serikali ya Sudan na waasi wa jimbo la Kordofan Kusini wanajadili pendekezo la kusitisha mapigano, liliyotolewa na wasuluhishi wa Umoja wa Afrika, ili kuyapa nafasi mashirika ya kutoa misaada kuwahudumia raia zaidi ya milioni moja.

Wasuluhishi wametoa pendekezo hilo juzi jumatatu huku wakiitaka serikali ya Khartoum na waasi kuliheshimu. Pande hizo mbili zimekua zikilaumiana kila mmoja kukwamisha mazungumzo.

Mazungumzo kati ya Khartoum na waasi yanalenga kusitisha kwa mapigano, ambayo yamedumu kwa miaka mitatu sasa katika majimbo ya Kordofan na Nil, machafuko ambayo yamewagusa raia zaidi ya milioni moja.

Hadi sasa haijajulikana idadi ya watu waliyopoteza maisha katika majimbo ya Kordofan na Nil.

Kwa mujibu wa Umoja wa mataifa, watu milioni 1.2 wameguswa na machafuko hayo au walilazimika kuyahama makaazi yao.