UGANDA

Uganda yapuuza vitisho vya mataifa ya Magharibi baada ya kupitisha sheria kali dhidi ya ushoga

Msemaji wa serikali ya Uganda Ofwono Opondo
Msemaji wa serikali ya Uganda Ofwono Opondo www.redpepper.co.ug

Serikali ya Uganda imepuuzilia mbali kauli za vitisho na hatua ambazo zimeanza kuchukuliwa na mataifa ya magharibi kusitisha misaada yao kwa nchi hiyo kutokana na kupitisha sheria kali inayokataza vitendo vya ushoga, ikisema inaweza kujiendesha hata bila kutegemea mataifa ya Ulaya. 

Matangazo ya kibiashara

Msemaji wa Serikali ya Uganda, Ofwono Opondo, amewaambia waandishi wa habari mjini Kampala kuwa nchi yao haitishwi na mataifa ya magharibi kwa kukatisha misaada yao kwa sababu ya kukataa ushoga na kuongeza kuwa nchi yake itaendelea kujiendesha hata bila ya misaada yao.

Kauli ya Uganda inakuja kufuatia benki ya dunia kutangaza kusitisha msaada wa fedha kwa nchi ya Uganda uliokuwa unafikia kiasi cha dola milioni 90 kwa ajili ya kuboresha sekta ya afya nchini humo.

Nchi za magharibi zimeendelea kutishia kusitisha misaada yao kwa nchi ya Uganda baada ya kupitishwa kwa sheria mpya ya kupiga marufuku wanaoendeleza mapenzi ya jinzia moja huku wadadisi wa maswala ya kiuchumi wakisema huenda nchi hiyo ikakumbwa na wakati mgumu.