Syria-Uchaguzi

Syria:Assad ashinda uchaguzi wa rais licha ya upinzani kuususia

Bachar el-Assad na mkewe Asma el-Assad wakipiga kura jiji Damascua Juni 3 2014 katika uchaguzi wa rais
Bachar el-Assad na mkewe Asma el-Assad wakipiga kura jiji Damascua Juni 3 2014 katika uchaguzi wa rais REUTERS/SANA

Rais wa Syria Bachar Al Assad ameibuka mshindi katika uchaguzi uliofanyika hivi majuzi kwa kujipatia asilimia 88.7 ya kura katika uchaguzi ambao umelaaniwa na jumuiya ya kimataifa, matokeo ambayo yanampa nguvu kuendeleza mapambano dhidi ya waasi.

Matangazo ya kibiashara

Kwa mujibu wa spika wa bunge la Syria, takriban watu milioni 11.6 dhidi ya milioni 15.8 ndio walioshiriki uchaguzi huo uliofanyika katika kipindi hiki cha miaka mitatu ya machafuko.

Saa chache kabla ya kutangazwa kwa matokeo hayo waziri wa mambo ya nje wa Marekani John Kerry akiwa ziarani jirani na syria nchini Lebanon amesema uchaguzi huo haukubaliki na kuwatolea wito washirika wa Syria kuhakikisha wanaung'oa utawala wa Assad.

Katika hatuwa nyingine, raia 30 wa Ufaransa waliojiunga na makundi ya uasi nchini Syria wamepoteza maisha katika mapambano. Hayo yamefahamishwa jana jioni na rais wa Ufaransa Franncois Hollande. Hollande amesema katika mkutano na vyombo vya habari wakati wa mkutano wa nchi 7 tajiri duniani kwamba swala hili linahitaji ushirikiano wa kutosha hususan katika nyanja ya kiitentelijensia.

Hollande amesema wameamuwa kushirikiana katika kupiga vita, kukomesha na kuadhibu harakati hizi ambazo zinaweza kuhatarisha usalama wa nchi husika, na kugusia shambulio la Mei 24 katika jumba la makumbusho ya kiyahudi jijini Brussels ambapo raia mmoja wa Ufaransa ambaye alipewa mafunzo nchini Syria alihusika.

Kwa mujibu wa takwimu zilizotangazwa mwezi April mwaka huu na viongozi wa serikali ya Ufaransa, takriban vijana 300 wanashukiwa kuwa wamejiunga na wapiganaji na wengine mamia wapo njiani kuelekea katika maeneo yanayomilikiwa na waasi na wengine wanashukiwa kuwa tayari wamerejea kutoka nchini Syria.