KOMBE LA DUNIA BRAZIL 2014

Cameroon yaanguka kwenye mchezo wake wa kwanza, Uholanzi yafanya mauaji kwa Uhispania

Nahodha wa Cameroon, Samuel Eto'o akishika kichwa baada ya timu yake kukosa bao dhidi ya Mexico
Nahodha wa Cameroon, Samuel Eto'o akishika kichwa baada ya timu yake kukosa bao dhidi ya Mexico REUTERS/Jorge Silva

Wawakilishi wa Afrika kwenye michuano ya mwaka huu timu ya taiafa ya Cameroon, jana Ijumaa imeanza vibaya michuani hii baada ya kukubali kipigo cha bao moja kwa sifuri dhidi ya Mexico, huku kwenye mchezo mwingine, Uholanzi wakaifanyia mauji ya kufuru mabingwa watetezi wa kombe hili, timu ya taifa ya Uhispania kwa kuwafunga mabao 5-1. 

Matangazo ya kibiashara

Mchezo kati ya Cameroon na Mexico ulicheza majira ya saa moja za usiku kwa saa za hapa Afrika mashariki, mchezo ambao macho na masikio ya waafrika wengi yalikuwa ni kwa timu ya Cameroon kuona kama wangeweza kufurukuta dhidi ya Mexico.

Kwenye mchezo huu, vijana wa Simba wasiofugika, Cameroon walianza vizuri kwa kutawala katika kipindi cha kwanza hasa dakika kumi za mwanzo, ambapo mshambuliaji mkongwe wa timu hii Samuel Eto'o alikosa mabao kadhaa ambayo yangeweza kuipa ushindi wa mwanzo timu hii.

Kutokuwa makini kwa mabeki wa Cameroon na hasa kwenye safu ya kiungo, kuliwafanya vijana wa Mexico waliokuwa wakiongozwa na Miguel Arturo, Héctor Miguel pamoja na José Juan Vázquez Gómez walitawala sehemu ya kiungo ya Mexico na kumbana Alexender Song wa cameroon kuweza kupitisha mipira ya uhakika kumfikia Samuel Eto'o.

Peralta akifunga bao la ushindi kwa timu yake ya Mexico ilipocheza na Cameroon
Peralta akifunga bao la ushindi kwa timu yake ya Mexico ilipocheza na Cameroon REUTERS/Carlos Barria

Mara baada ya kwenda mapumziko bila ya timu hizo kufungana, timu hizi zilirejea kwenye kipindi cha pili kwa kasi ambapo Mexico walizidisha mashambulizi ambayo yaliwawezesha kuandika bao lao la kwanza kwenye dakika ya 61 ya mchezo, bao lililofungwa na Oribe Peralta akiunganisha mpira wa pasi.

Kwenye mchezo huu ambao Cameroon walikuwa na bahati ya kutofungwa mabao mengi kutokana na uzembe wa mabeki wake ambao walikuwa wakijisahau muda mwingi, mfano mzuri ni mabao mawili wa Giovan Dos Santos ambayo yalikataliwa na mwamuzi kwa madai kuwa alikuwa ameotea wakati akitaka kufunga.

Mashabiki wa Mexico wakishangilia ushindi wa timu yao
Mashabiki wa Mexico wakishangilia ushindi wa timu yao REUTERS/Jorge Silva

Maamuzi tata ya mwamuzi, Wilmar Alexander Roldán Pérez wa Colombia yaliwafanya hata wakati fulani wachezaji wa Mexico pamoja na kocha wao Miguel Herrera kumbwatukia mwamuzi mara kwa mara kutokana na maamuzi ambayo alikuwa akiyafanya.

Mpaka mwamuzi huyu anapuliza kipyenga cha mwisho kumaliza mchezo huu, Cameroon walilala kwa bao 1-0 dhidi ya Mexico ambao walivunja mwiko wa kushindwa kutamba mbele ya timu za Afrika.

Mchezo mwingine ulipigwa maajira ya saa nne za usiku kwa saa za hapa Afrika mashariki ambapo Uholanzi walikuwa na kibarua dhidi ya mabingwa watetezi wa kombe hilo, timu ya taifa ya Uhispania.

Mshambuliaji wa Uholanzi, Robin van Persie akifunga bao la kusawazisha dhidi ya Uhispania
Mshambuliaji wa Uholanzi, Robin van Persie akifunga bao la kusawazisha dhidi ya Uhispania REUTERS/Michael Dalder

Kwenye mchezo huu ambao wengi walikumbuka fainali za mwaka 2010 nchini Afrika Kusini wakati timu hizi zilizpocheza fainali, ulikuwa ni mchezo ambao kila mmoja alitarajia kuona unakuwa wa ushindani kwa muda wote wa mchezo.

Uhispania kama ilivyo ada wakiongozwa na viungo mahiri duniani, Xavi, Iniesta na Alonso walitawala kipindi cha kwanza kwa kutoa pasi za uhakika kwa washambuliaji wake waliokuwa wakiongozwa na Diego Costa mwenye asili ya Brazil lakini akachukua uraia wa Uhispania.

Xabi Alonso wa Uhispania akifunga bao la kwanza la timu yake dhidi ya Uholanzi
Xabi Alonso wa Uhispania akifunga bao la kwanza la timu yake dhidi ya Uholanzi REUTERS/Marcos Brindicci

Walikuwa ni Uhispania ambao walikuwa wa kwanza kuandika bao kwenye dakika ya 27 ya mchezo, bao likifungwa na Xabi Alonso kwa njia ya panati, penati iliyopatikana baada ya mchezaji Diego Coasta kuangushwa kwenye eneo la hatari.

Bao hilo liliwafanya Uhispania kushambulia kwa nguvu zaidi kutaka kupata ao la nyongeza, lakini juhudi zao hazikufua dafu kwani kwenye dakika ya 44 ya mchezo, mshambuliaji wa Manchester United, Robin van Persie alifanikiwa kuisawazishia timu yake bao kwa kuopiga kichwa cha kiufundi akipokea pasi kutoka winga ya kushoto.

Arjen Robben wa Uholanzi akifunga bao la nne kwa timu yake dhidi ya Uhispania
Arjen Robben wa Uholanzi akifunga bao la nne kwa timu yake dhidi ya Uhispania REUTERS/Michael Dalder

Timu hizo zilienda mapumziko zikiwa sare ya bao 1-1, kipindi cha pili kilianza kwa kasi zaidi na kwa mara nyingine walikuwa ni Uholanzi ambao walitangulia kupata bao kupitia kwa van Persie tena ambaye alitumia makosa ya mlinda mlango wa Uhispania, Iker Casilas ambaye alishindwa kuumudu mpira aliorejeshewa na beki wake na kumpa nafasi Van Persie kumpokonya na kupachika kwenye kimia kuandika bao la pili.

Wakati Uhispania wakiendelea kujipanga kutaka kurejesha bao hilo, dakika ya 53 kiungo wa pembeni, Arjen Roben aliiandikia timu yake bao la tatu, kabla ya De Vriji kuandika bao la nne kwenye dakika ya 64 ya mchezo na kuzidi kuwachanganya wachezaji wa Uhispania ambao walikuwa hawaamini kinachotokea.

Van Persie akifunga bao la pili kwa timu yake baada ya kumzidi ujanja kipa wa Uhispania
Van Persie akifunga bao la pili kwa timu yake baada ya kumzidi ujanja kipa wa Uhispania REUTERS/Michael Dalder

Aliyepigilia msumari wa mwisho na watano kwenye jeneza la mabingwa watetezi hakuwa mwingine bali ni Arjen Roben ambaye aliwazidi akili mabeki na kipa wa Uhispania ambae alishindwa kumzua na kupigwa chenga ambayo baadae Roben akapachika kwenye nyavu kwa mguu wake wa kushoto kuandika bao la 5 na la ushindi kwa timu hiyo.

Mara baada ya mchezo huo hakuna aliyeamini kuwa mabingwa watetezi timu ya taifa ya Uhispania ilikubali kichapo cha mabao 5-1.

Kocha wa Uhispania, Vicente Del Bosque alikuwa mpole baada ya kumalizika kwa mechi hiyo, ambapo muda mwingi alikuwa akiwafariji wachezaji wake ambao walionekana kutokwa na machozi wasiamini kile kilichowakuta kwenye mechi ya ufunguzi.

Mchezo wa mwisho kwenye kundi B ulipigwa majira ya saa saba za usiku kwa saa za hapa Afrika mashariki, ambapo vijana wa Chile walikuwa na kibarua dhidi ya Australia, kwenye mchezo ambao umeshuhudia Chile wakifanikiwa kuchomoza na ushindi wa mabao 2-1 kwa moja.

Bao la kwanza la kwanza la Chile lilipatikana kwenye dakika ya 12 ya mchezo likifungwa na Alexis Sanchez kabla ya dakika mbili baadae mchezaji Jorge Toro kuiandikia timu yake bao la pili na laushindi kwenye mchezo ambao hakika Chile alionesha toka awali kutaka kupata ushindi wa mapema.

Timu ya taifa ya Australia walifanikiwa kupata bao lao la kufutia machozi kwenye dakika ya 35 ya mchezo likiwekwa kimiani na mkongwe Tim Cahil ambaye baada ya kuwazidi ujanja mabeki wa Chile aliachia shuti kali ambalo lilijaa moja kwa moja kwenye goli.

Hata hivyo timu zote mbili lazima zijilaumu kwa kukosa mabao mengi ya wazi kwenye kipindi cha kwanza na hata cha pili, ambapo kama ingekuwa washambuliaji wake wako makini wangeweza kuziopa ushindi timu zao.

Hii leo kutakuwa na mechi kadhaa ambazo zitapigwa, ambapo timu ya taifa ya Colombia itakuwa na kibarua dhidi ya Ugiriki, wakati Uruguay watakuwa na kibarua dhidi ya Costa Rica, Uingereza watakuwa na kibarua dhidi ya Italia na Japan watakuwa na kibarua na wageni kutoka bara la Afrika Tembo wa Ivory Coast.

Mechi zote hizi ni za kundi C na D kwa pamoja.