KOMBE LA DUNIA BRAZIL 2014

Ghana yaangukia pua huku Nigeria ikiambulia sare wakati Ujerumani ikiiadhibu Ureno, leo ni zamu ya Algeria

Mlinda mlango wa timu ya taifa ya Nigeria, Vincent Enyeama akiokoa mpira uliokuwa unaelekea langoni mwake
Mlinda mlango wa timu ya taifa ya Nigeria, Vincent Enyeama akiokoa mpira uliokuwa unaelekea langoni mwake REUTERS/Ivan Alvarado

Timu ya taifa ya Nigeria na Ghana ambao ni wawakilishi wengine toka barani Afrika hapo jana zimeshindwa kutamba kwenye mechi zao za ufunguzi kwenye fainali za kombe la dunia, baada ya Nigeria kutoka suluhu na Iran huku Ghana ikifungwa na Marekani. 

Matangazo ya kibiashara

Kwenye mchezo huo wa kudni F ulishuhudia tomu zote mbili zikifanya mashambulizi ya kushtukiza huku washambuliaji wakishindwa kutumia vema nafasi walizokuwa wakizipata na ambazo zingeweza kubadili matokeo ya mchezo.

mchezaji wa Nigeria akiwa amebanwa na wachezaji wawili wa Iran
mchezaji wa Nigeria akiwa amebanwa na wachezaji wawili wa Iran REUTERS/Amr Abdallah Dalsh

Nigeria iliyokuwa ikiongozwa na nahodha Josephu Yobo na Vicent Enyiama iklishindwa kabisa kuonesha makucha yake wala kuwa namashambulizi ya hatari kwenye lango la timu ya taifa ya Iran, hali ambayo mara nyingi kocha wake Stephen Keshi alionekana kukasirishwa na kiwango cha wachezaji wake.

Katika dakika ya 29 ya mchezo, kocha Stephen Keshi alilazimika kumtoa mchezaji wake Oboabina aliyeumia na nafasi yake kuchukuliwa na nahodha Josephu Yobo, na kumtoa tena Victor Moses na kumuingiza Shola Ameobi, huku Peter Odemwingie akichukua nafasi ya Azeez kwenye mabadiliko ambayo hata hivyo hayakuzaa matunda.

Ahmed Musa wa timu ya taifa ya Nigeria akijaribu kufunga langoni mwa Iran
Ahmed Musa wa timu ya taifa ya Nigeria akijaribu kufunga langoni mwa Iran REUTERS/Amr Abdallah Dalsh

Kwa upande wa kocha wa Iran, Carlos Queiroz alifanya mabadiliko mawili pekee ambapo alimuingiza Jahanbakhsh aliyechukua nafasi ya Dejagah huku Shojeai akichukua nafasi ya Heydari, mabadiliko ambayo nayo pia hayakuzaa matunda.

Mpaka mwisho wa mchezo huo timu hizi zilitoka sare ya bila kufungana.

Mchezo mwingine uliowashuhudiwa wawakilishi wengine wa Afrika ni mechi za kundi G ambapo timu ya taifa ya Ghana walikuwa na kibarua dhidi ya Marekani, kwenye mchezo ambao ulishuhudia wawakilishi hawa wa Afrika wakishindwa kutamba na kukubali kichapo cha mabao 2-1.

Kwenye mchezo huo ambao Ghana itabidi wajilaumu wenyewe kwa kuruhusu wachezaji wa timu ya taifa ya Marekani kulikaribia lango lao mara kwa mara, walikuwa na kila sababu ya kuhakikisha wanapata ushindi kwenye mechi hii.

Marekani ndio waliokuwa wa kwanza kupata bao katika dakika ya kwanza tu ya mchezo likifungwa na nahodha Clint Dempsey ambaye kwa kutumia uzoefu wake, aliwapiga chenga mabeki wa Ghana waliomuachia mpaka akaingia kwenye eneo la hatari na kuachia shuti lililotinga moja kwa moja nyavuni.

André Ayew akiifungia timu yake ya Ghana bao la kusawazisha dhidi ya Marekani, Ghana ilifungwa mabao 2-1
André Ayew akiifungia timu yake ya Ghana bao la kusawazisha dhidi ya Marekani, Ghana ilifungwa mabao 2-1 REUTERS/Carlos Barria

Kipindi cha kwanza kilimalizika kwa timu ya taifa ya Marekani kuongoza kwa 1-0, ambapo kipindi cha pili kilianza kwa kasi na timu ya taifa ya Ghana ilifanikiwa kusawazisha bao hilo kupitia kwa Andrew Ayew katika dakika ya 82 baada ya kutumia vema mpira aliopigiwa na nahodha Asamoah Gyan.

Wakati Ghana wakizidisha mashambulizi na kujaribu kutafuta walau bao la ushindi, walijikuta wakiruhusu mashambulizi ya hatari langoni mwao, ambapo katika dakika ya 86 ya mchezo, Marekani walipata kona iliyowasaidia kupata bao lililowekwa kimiani na mchezaji John Brooks kufuatia kona iliyopiga na Graham Zusi.

Kwa matokeo haya sasa ni wazi Ghana watalazimika kushinda mchuano wao unaofuata ambao utakuwa dhidi ya timu ya taifa ya Ureno ambayo nayo ilipoteza mchezo wake dhidi ya Ujerumani kwenye mchezo mwingine wa kundi G.

Katika mchezo mwingine wa kundi hili, timu ya taifa ya Ujerumani wao waliwakaribisha timu ya taifa ya Ureno lwenye mchezo ambao ulitoa matokeo ya kushangaza baada ya wajerumani kuwafunga Ureno kwa jumla ya mabao 4-0 huku mchezaji Thomas Muller akifunga Hatrick ya kwanza kwenye michuano ya mwaka huu.

Kwenye mchezo huu ambao ni wazi kabisa Ujerumani waliwazidi kimchezo Ureno katika kila idara, haikuwachukua muda kuandika bao la kuongoza kwa njia ya tuta, bao lililofungwa na Thomas Muller.

Baada ya bao hili, Ujerumani walizidisha mashambulizi ambapo katika dakika ya 32 ya mchezo, mchezaji Mats Hummels aliiandikia timu yake bao la pili baada ya kutumia vema mpira wa pasi aliopewa Toni Kroos, dakika 16 baadae Ujerumani walifanikiwa kupata bao la tatu likifungwa tena na Thomas Muller katika dakika za nyongeza kabla ya kwenda mapumziko.

Mshambuliaji wa Ujerumani, Thomas Müller akiifungia timu yake bao la 4 dhidi ya Ureno
Mshambuliaji wa Ujerumani, Thomas Müller akiifungia timu yake bao la 4 dhidi ya Ureno REUTERS/Fabrizio Bensch

Bao la mwisho la Ujerumani liliwekwa kimiani na mshambuliaji Thomas Muller tena ambaye alihitimisha karamu hii ya magoli dhidi ya Ureno na kuwa mchezaji wa kwanza kabisa kufunga mabao matatu katika mechi moja.

Wachezaji wa Ureno waliokuwa wakiongozwa na mchezaji bora wa dunia na nahodha wa timu hiyo Christian Ronaldo walishindwa kabisa kufurukuta mbele ya Ujerumani ambayo ilishuhudiwa pia na kansela wao, Angela Merkel.

Leo kutakuwa na mechi nyingine za kundi H ambapo wawakilishi wengine wa Afrika timu ya taifa ya Algeria watatupa karata yao ya kwanza kwa kucheza na Ubelgiji, kwenye mchezo ambao Ubelgiji wanapewa nafasi kubwa zaidi ya kuweza kushinda mchezo huu.

Mechi nyingine ya kundi hili ni ule utakaozikutanisha timu ya taifa ya Urusi itakayokuwa na kibarua dhidi ya Jamhuri ya Korea, mchezo ambao utapigwa majira ya saa saba za usiku wa kuamkia Jumanne.

Mechi nyingine ambayo itachezwa hivi leo ni ile ya kundi A ambapo wenyeji Brazil watacheza mchezo wao wa pili kwa kucheza na timu ya Taifa ya Mexico, mchezo huu ni muhimu kwa timu zote mbili kwakuwa wote walishinda mechi zao za awali.