KOMBE LA DUNIA BRAZIL 2014

Ujerumani yatawazwa mabingwa kombe la dunia 2014, Messi awa mchezaji bora wa michuano

Wachezaji wa Ujerumani wakishangilia baada ya kukabidhiwa kombe la dunia
Wachezaji wa Ujerumani wakishangilia baada ya kukabidhiwa kombe la dunia fifa.com

Timu ya taifa ya Ujerumani siku ya Jumapili ilitawazwa kuwa mabingwa wapya wa kombe la dunia kwa mwaka 2014 nchini Brazil, ikiwa ni taji lake la nne kufuatia ushindi wa lala salama iliyoupata dhidi ya timu ya taifa ya Argentina.  

Matangazo ya kibiashara

Ujerumani ilitawazwa mabingwa kufuatia bao lililofungwa kwenye muda wa nyongeza na mshambuliaji kinda wa Ujerumani Mario Gotze ambaye alitumia vema uzembe wa mabeki wa Argentina walioshindwa kumdhibiti na kupachika mpira kwenye kimia.

Dakika tisini za mchezo huu zilimalizika bila timu kuona lango la mwenzake huku wachezaji wa timu zote mbili wakikosa nafasi za wazi ambazo zingeweza kuzipatia timu zao ushindi.

Kipindi cha kwanza Gonzalo Higuan alipata nafasi ambayo ataijutia baada ya kupata mpira kwenye eneo la Ujerumani na kubaki na kipa wa Ujerumani Manuel Nuer na kushindwa kupachika mpira kwenye kimia.

Mchezaji Lionel Messi naye katika kipindi cha pili alifanikiwa kupata nafasi kadhaa za wazi ambao angekuwa makini huenda angeipa timu yake ushindi na kufanikiwa kutwaa taji la mwaka huu.

Mabeki wa Ujerumani wakiongozwa na nahodha wa timu hiyo Philip Lahm walifanya kazi kubwa na yaziada kuwazuia washambuliaji wa Argentina ambao mara kadhaa walijaribu kuupita ukutwa wa wajerumani bila mafanikio.

Kufuatia ushindi wa hapo jana, timu ya taifa ya Ujerumani iliyokuwa inaongozwa na kocha Joachim Low imekuwa ni timu ya kwanza kutoka kwenye ukanda wa Ulaya kufanikiwa kuchukua taji hilo kwenye ardhi ya bara la America.

Kwenye mchezo wa hapo jana Ujerumani ilikosa huduma za mchezaji wake Sami Khedira ambaye alipata majeraha wakati wa mazoezi ya timu yake siku moja kabla ya mchezo ambapo nafasi yake ilichukuliwa na kinda Christoph Kramer ambaye nae alishindwa kumaliza mchezo huo baada ya kuumia kichwa.

Shirikisho la kabumbu duniani fifa kabla ya kutoa kombe hilo kwa Ujerumani iliwatangaza wachezaji waliofanya vizuri kewenye michuano hiyo, akiwemo Lionel Messi aliyeshinda taji mchezaji bora wa michuano.

James Rodriguez wa Colombia alichukua kiati cha dhahabu baada ya kufanikiwa kuwa mfungaji bora wa mashindano ya mwaka huu, huku mlinda mlango bora wa mashindano akiwa ni kipa wa Ujerumani Manuel Nuer.

Mchezaji chipukizi wa mashindano hayo alikuwa ni mshambuliaji wa Ufaransa, Pogba, huku timu yenye nidhamu ikiwa ni timu ya taifa ya Costa Rica.