KOMBE LA DUNIA BRAZIL 2014

Timu ya taifa ya Ujerumani yapokelewa kishujaa ikirejea kutoka Brazil

mashabiki wa soka wakiwa wamelizunguka gari lililowabeba wachezaji wa timu ya taifa ya Ujerumani
mashabiki wa soka wakiwa wamelizunguka gari lililowabeba wachezaji wa timu ya taifa ya Ujerumani fifa.com

Maelfu ya mashabiki wa timu ya taifa ya Ujerumani hii leo walifurika kwenye barabara za jiji la Berlin katika eneo la Brandenburg Gate kuwakaribisha nyumbani wachezaji wa timu hiyo ambao wamerejea kutokea nchini Brazil baada ya kutawazwa kuwa mabingwa wapya wa kombe la dunia lililomalizika mwishoni mwa juma nchini Brazil. 

Matangazo ya kibiashara

Mapokezi haya yamekuwa makubwa zaidi kuwahi kushuhudiwa kwa timu hiyo, ambapo safari hii mashabiki wa soka kutoka kila pembe ya Ujerumani bila kujali eneo wanakotoka walikusanyika kwa pamoja kuwapokea mashujaa wao.

Basi lililowabeba wachezajiw a Ujerumani likiwa limezingirwa na mashabiki waliojitokeza kuwakaribisha nyumbani.
Basi lililowabeba wachezajiw a Ujerumani likiwa limezingirwa na mashabiki waliojitokeza kuwakaribisha nyumbani. fifa.com

Maelfu ya raia wakiwa na bendera ya taifa na jezi za timy yao ya taifa walianza kufurika kwenye viwanja hivyo saa chache kabla ya wachezaji wa timu hiyo kuwasili wakitokea jijini Rio De Jeneiro.

Kocha mkuu wa timu hiyo, Joachim Loew akiwahutubia maelfu ya mashabiki waliofurika kuwapkea vijana wake, amesema kuwa hizi ni sherehe kubwa na tukio muhimu kwenye historia ya taifa hilo ambalo limewaunganisha wajerumani wote.

Wachezaji wa Ujerumani wakiwa kwenye picha ya pamoja baada ya kukabidhiwa kombe la dunia
Wachezaji wa Ujerumani wakiwa kwenye picha ya pamoja baada ya kukabidhiwa kombe la dunia REUTERS/Michael Dalder

Joachim anasema "Sote ni washindi wa dunia, na kusema kweli sote tunafuraha kupita kiasi na hasa upande wetu kwakuwa tuko nanyi mashabiki wetu" alisema kocha huyo.

Nahodha wa timu hiyo, Philip Lahm kwa mara nyingine alipata fursa ya kulinyanyua kombe la dunia mbele ya maelfu ya mashabiki ambao punde baada ya kujitokeza kwa mashabiki hao walipiga kelele za kushangilia kuonesha kuwaunga mkono wachezaji wao.