MSUMBIJI-RENAMO-FRELIMO-Uchaguzi-Siasa

Msumbiji: hali ya wasiwsi yatanda, Renamo yajitangazia ushindi

Mji mkuu wa Msumbiji, Maputo.
Mji mkuu wa Msumbiji, Maputo. Wikimedia

Nchini Msumbiji, chama cha upinzani Renamo kimejitangazia ushindi wa uchaguzi wa urais, na kukataa kukubali matokeo yanayotangazwa na tume ya Uchaguzi yanayoenekana kukipa ushindi chama tawala cha Frelimo.

Matangazo ya kibiashara

Msemaji wa Renamo, Antonio Muchanga, amesema hawawezi kutambua matokeo hayo, kauli ambayo inazua hali ya wasiwasi ya kutokea kwa machafuko baada ya matokeo ya mwisho kutangazwa.

Hadi sasa, robo ya kura zote zimekwishahesabiwa na mgombea wa Frelimo Filipe Nyusi anaongoza kwa asilimia 63 akifuatwa na mgombea wa Renamo Afonso Dhlakama ambaye ana asilimia 30.

Matokeo ya mwisho yanatarajiwa mwishoni mwa juma hili.

Chama cha Renamo kimekua kikikosoa namna zoezi la uhesabuji kura lilivyoendeshwa, kikibaini kwamba zoezi hilo liligubikwa na kasoro nyingi.

Chama cha Renamo kilikubali kushiriki uchaguzi mwezi uliyopita, baada ya kutia saini kwenye mkataba wa amani ambao ulisitisha mapigano kati ya utawala uliokueko madarakani kabla ya uchaguzi na chama hicho cha Renamo.

Mwanzoni mwa juma hili, kiongozi wa chama cha Renamo, Afonso Dhlakama aliielezea matumaini yake kwamba kwa mara ya kwanza matokeo yataheshimishwa na yatakua ya wazi.

Hata hivo waangalizi wa Umoja wa Ulaya wamebaini kwamba uchaguzi pamoja na zoezi la uhesabuji wa kura viliendeshwa katika hali ya utulivu na uwazi, hata kama kulikueko na baadhi ya kasoro.

Hali ya wasiwasi imetanda leo Ijumaa nchini kote Msumbiji, raia wakihofia kutokea tena kwa machafuko kama yale yaliyotokea miaka iliyopita.