VANUATU

Hali ya hatari yatangazwa katika kisiwa cha Vanuatu

Hali ya hatari imetangazwa katika kisiwa cha Vanuatu kinachopatikana Kusini mwa Bahari ya Pacific baada ya kutokea kwa kimbuga kikali hapo mwishoni mwa juma hili na kusababisha vifo vya watu wanane na kusababisha uharibu mkubwa wa mali.

Kisiwa katika kisiwa cha Vanuatu
Kisiwa katika kisiwa cha Vanuatu REUTERS/UNICEF Pacific/Handout via Reuters
Matangazo ya kibiashara

Kwa sasa hakuna kinachoendelea katika mji mkuu Port Vila na watu wanaonekana wakiwa wamesimama barabarani bila ya kupata msaada wowote na maelfu wamelazimika kulala nje baada ya maakazi yao kuharibiwa.

Rais Baldwin Lonsdale akizungumza katika mkutano wa Kimataifa nchini Japan siku ya Jumamosi, ameiomba Jumuiya ya Kimataifa kuisaidia nchi yake na kuwasaidia wananchi wake ambao wana mahitaji mengi kwa sasa.

Rais Lonsdale amesema ” nazungumza nanyi kwa moyo mzito sana, na sijui kimbuga hiki kitatuathiri hadi lini, nawaomba mtusaidie ili wananchi wetu wapate afueni.”

Tayari Umoja wa Mataifa, New Zealand, Australia na Uingereza zimeahidi kutoa kwa Kisiwa hicho kutokana na kimbuga hiki kibaya kuwahi kutokea katika nchi hiyo ndogo yenye zaidi ya watu Laki Mbili.

Mambo muhimu yanayohitajika kwa sasa katika kisiwa hicho ni ujenzi wa makazi ya watu waliokimbia makwao, maji safi ya kunywa pamoja na chakula.