MEI MOSI-HALI-MAANDAMANO

Mei Mosi: maandamano duniani, hali ya taharuki Istanbul na Paris

Hali jinsi ilivyokua kwenye eneo la Jamhuri, Ufaransa, Mei 1, 2016.
Hali jinsi ilivyokua kwenye eneo la Jamhuri, Ufaransa, Mei 1, 2016. ALAIN JOCARD / AFP

Siku ya Mei mosi ilisheherekewa katika nchi mbalimbali duniani lakini katika baadhi ya nchi kulishuhudiwa makabiliano kati ya polisi na waandamanaji wakipinga hali duni ya maisha inayowakabili pamoja na mishahara finyu. Siku hiyo ilikumbwa na hali ya sintofahamu katika mji mkuu wa Uturuki, Istanbul na Paris nchini Ufaransa.

Matangazo ya kibiashara

Mjini Istanbul, polisi walitumia mabomu ya machozi na mizinga ya kurusha maji kuwatawanya waandamanaji katika maeneo kadhaa katika mji huo mkuu wa Uturuki, hasa karibu na eneo maarufu la Taksim, kitovu cha maandamano.

Mbali na makabiliano hayo kati ya polisi na waandamanaji, mtu mmoja alipoteza maisha baada ya kugongwa kwa gari la kikosi cha kutuliza ghasia, alipokua akivuka barabara katikati ya mji, polisi imesema. Zaidi ya watu 200 ambao walikuwa wakijaribu kuandamana katika eneo la Taksim walikamatwa, kwa mujibu wa mkuu wa mji.

Wafuasi wa chama cha HDP kinachounga mkono Wakurdi walitawanywa pia vikali na polisi, ambapo askari polisi 25,000 walishiriki katika operesheni hiyo na kuzingira mitaa mingi kwa kujiandalia siku hiyo ya wafanyakazi duniani, ambayo mara nyingi inakumbwa na makabiliano kati ya wafuasi wanaopinga utawala na vikosi vya usalama.

Nchini Ufaransa, Sikukuu ya kazi na wafanyakazi ilisherehekewa katika hali ya mvutano, baada ya miezi miwili ya maandamano dhidi ya muswada wa sheria ya kazi na maandamano mengi yenye vurugu.

Maelfu ya watu, 84,000 kwa mujibu wa mamlaka, waliandamana nchini kote, wakidai muswada huo utakaojadiliwa katika Bungekuanzia Jumanne hii, uondolewa Bungeni. Katika mji wa Paris, kati ya waandamanaji 16,000 kwa mujibu wa polisi, hadi 70,000 kwa mujibu wa vyama vya wafanyakazi, walimiminika mitaani Jumapili mchana chini ya ulinzi mkali wa polisi, wakati wa gwaride la kipekee la vyama vya wafanyakazi, ikiwa ni mara ya kwanza tangu miaka saba iliyopita.

Katika maeneo mbalimbali nchini Ufaransa maandamano yaliendelea hadi saa mbili usiku, huku polisi ikijaribu kuwatawanya kwa kutumia mabomu ya machozi.

Nchini Urusi, karibu watu 100,000 kwa mujibu wa polisi walishiriki katika gwaride mjini Moscow lililofanyika katika eneo jekungu (Red Square). Nchini Poland, msafara wa maelfu ya waandamanaji walishiriki gwaride kwa amani katika mji wa Warsaw.

mjini Madrid, watu elfu kadhaa, ikiwa ni pamoja viongozi wa Chama cha Kisosholisti Pedro Sanchez na Izquierda Unida Alberto Garzon, walishiriki maandamano yalioongozwa na vyama vikuu viwili vya wafanyakazi CCOO na UGT, ambavyo vilikua vimebebelea bango lililoandikwa "dhidi ya mshahara na umaskini katika jamii, wafanyakazi na haki za binadamu. "