KOREA KASKAZINI

UN yaimarisha vikwazo dhidi ya Korea Kaskazini

Rais wa Korea Kaskazini Kim Jong Un akizuru makaburi ya kivita katika sherehe za miaka 64  tangu kumalizika kwa vita ya Korea July 28, 2017
Rais wa Korea Kaskazini Kim Jong Un akizuru makaburi ya kivita katika sherehe za miaka 64 tangu kumalizika kwa vita ya Korea July 28, 2017 Reuters/路透社

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa jana Jumamosi kwa pamoja limeunga mkono azimio lililoandaliwa na Marekani ambalo linaimarisha kwa kiasi kikubwa vikwazo kwa Korea Kaskazini, na kupiga marufuku mauzo ya nje ya nchi kwa lengo la kuinyima Pyongyang dola bilioni 1 katika mapato ya kila mwaka.

Matangazo ya kibiashara

Hatua hizo ni za kwanza za aina hiyo kuchukuliwa dhidi ya Korea ya Kaskazini tangu Rais wa Marekani Donald Trump achukue mamlaka na zinaonyesha nia ya China kumuadhibu mshirika wake Pyongyang.

Rais Trump, amepongeza hatua za China na Urusi kuunga mkono vikwazo hivyo vilivyotolewa na baraza hilo la Umoja wa mataifa na kusema kuwa, vikwazo hivyo, vitakuwa na "athari kubwa mno" ya kibiashara.

Majirani wao Korea Kusini, wameiomba Korea Kaskazini kufuata njia ya mazungumzo, ili kutanzua mzozo uliopo wa mpango wa Pyongyang, kuhusu zana za kinyuklia.

Aidha nchi ya Beijing pia inaomba kurejelewa kwa mazungumzo.

Azimio limezuia kabisa mauzo ya makaa ya mawe, chuma, risasi pamoja na samaki na baadhi ya vyakula ambayo hulipatia pato taifa hilo.