VENEZUELA-BRAZIL-UCHUMI

Wakimbizi wa Venezuela waendelea kukimbilia nchini Brazil

Raia wa Venezuela wakiingia nchini Brazil
Raia wa Venezuela wakiingia nchini Brazil AFP

Idadi ya raia wa Venezuela wanaokimbilia nchini Brazil, inaongezeka licha ya kushambuliwa katika kambi yao mwishoni mwa wiki iliyopita na kusababisha vifo vya watu 13 na wengine kujeruhiwa.

Matangazo ya kibiashara

Msemaji wa jeshi nchini Brazil amesema, siku ya Jumatatu, raia 900 wa Venezuela waliingia nchini humo na wapo katika jimbo la Rorarma.

Hali hii inaendelea kuleta wasiwasi kati ya mpaka wa Brazil na Venezuela, huku wakimbizi hao wakisema wanakimbia hali ngumu ya uchumi katka nchi yao.

Mwishoni mwa wiki iliyopita, serikali ya Brazil ilituma wanajeshi katika mpaka wake na Venezuela ili kuzuia mapigano kati ya wenyeji na raia hao wa Venezuela wanaoingia nchini humo.

Hatua ya serikali ya Venezuela kuchapisha noti mpya za fedha, kumewaacha wengi katika hali ngumu ya kiuchumi, lakini serikali ya rais Nicholas Maduro inasema imefanya hivyo ili kukabiliana na hali ngumu ya kiuchumi nchini humo.

Wanasiasa wa upinzani wamepanga maandamano hivi leo kupinga hatua hii.