DIEGO MARADONA-ARGENTINA

Gwiji wa soka, Diego Armando Maradona, afariki dunia

Diego Armando Maradona, gwiji wa soka aliyefariki Novemba 25, 2020. Katika picha ilikuwa ni Desemba 26, 2019 mjini Buenos Aires.
Diego Armando Maradona, gwiji wa soka aliyefariki Novemba 25, 2020. Katika picha ilikuwa ni Desemba 26, 2019 mjini Buenos Aires. Marcos Brindicci/AP Photo

Gwiji wa soka duniani, Diego Maradona, moja kati ya wachezaji wanaotajwa kuwa bora zaidi kuwahi kutokea, amefariki dunia akiwa na umri za miaka 60.

Matangazo ya kibiashara

Kiungo huyu mshambuliaji wa zamani wa timu ya taifa ya Argentina na pia aliwahi kuwa kocha, alipata mshtuko wa moyo, akiwa nyumbani kwake mjini Buenos Aires.

Maradona alifanyiwa upasuaji wa ubongo uliofanikiwa kwa kiwango kikubwa mwanzoni mwa mwezi Novemba ambapo pia alikuwa akipatiwa matibabu ya uraibu wa pombe.

Maradona alikuwa nahodha wa timu yake ya taifa ya Argentina, ambayo aliisaidia kutwaa taji la kombe la dunia mwaka 1986, akifunga goli kwa kutumia mkono, goli ambalo limeendelea kumpa umaarufu hadi umauti unamkuta.

Mshambuliaji wa klabu ya FC Barcelona na timu ya taifa ya Argentinam Lionel Messi, ameandika kwenye ukurasa wake wa kijamii, akisema ulimwengu wa soka umepoteza gwiji, na kwamba licha ya kuwa amefariki, lakini bado ataendelea kuishi.

Katika ukurasa wake wa kijamii, shirikisho la soka la Argentina, limeelewa kuguswa na kifo cha Maradona, taarifa yake ikisema ‘Siku wote utasalia mioyoni mwetu’.

Rais za Argentina, Alberto Fernandez, ametangaza siku tatu za maombolezo, akisema ‘ulitupeleka kombe la dunia, ulitupa furaha isiyokifani, hakika ulikuwa shujaa’.

Maradona aliwahi kuzichezea timu za FC Barcelona na Napoli, akishinda mataji mawili ya Seria A na Napoli.

Maradona alianza maisha ya soka na klabu ya Argentina ya Juniors, huku pia akichzea Sevilla, Boca Juniors na Newell’s Old Boys ya nchini mwake.

Alifunga magoli 34 na kuichezea tumu yake ya taifa mara 91, akishiriki kucheza michuano minne ya kombe la dunia.

Maradona aliisaidia timu yake kufika fainali za kombe la dunia nchini Italia mwaka 1990, ambapo walifungwa na iliyokuwa Ujerumani Magharibi, kabla ya kuiongoza tena timu yake wakati wa fainali za mwaka 1994 nchini Marekani, ambapo hata hivyo alirudishwa nyumbani baada ya kushindwa kufuzu vipimo vya kutambua ikiwa alitumia dawa za kusisimua misuli au la.

Akiwa katika awamu ya pili ya maisha yake ya soka, Maradona alikuwa mraibu wa dawa za kulevya aina ya Cocain, ambapo alifungiwa kwa miewi mitano baada ya kugundulika alitumia dawa hizo mwaka 1991.

aliamua kustaafu soka mwaka 1997, wakati akitimiza miaka 37 akiwa na klabu yake ya nyumbanim Boca Juniors.

Akiwa ameongoza vilabu viwili nchini mwake kwa nyakati tofauti, Maradona aliteuliwa kuwa kocha wa timu ya taifa ya Argentina mwaka 2008 na aliondoka kwenye nafasi hiyo baada ya fainali za mwaka 2010, ambapo timu yake ilifungwa na Ujerumani katika hatua ya robo fainali.

Pia alishawahi kufundisha timu za mataifa ya Falme za Kiarabu, Mexico na Gimnasia Esgrima ya Argentina hadi wakati umauti unamfika.