IMF-UCHUMI

IMF kuongeza dola bilioni 650 kwenye akiba yake ya dharura

Mkurugenzi wa Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF), Kristalina Georgieva.
Mkurugenzi wa Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF), Kristalina Georgieva. © RFI

Mkurugenzi wa Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF), Kristalina Georgieva, ametangaza kwamba atawasilisha kwa bodi ya wakurugenzi ya IMF pendekezo rasmi kuhusu uwezekano wa kuongeza dola bilioni 650 (euro bilioni 548) katika akiba ya mfuko wa dharura ifikapo mwezi Juni.

Matangazo ya kibiashara

Kristalina Georgieva amesema mgao mpya wa Haki Maalum (SDR) utazipa nchi wanachama - ambazo nyingi zimeathiriwa sana na janga la COVID-19 - nafasi ya kulipa madeni yao baada ya kupewa muda wa kutosha bila kuongeza mzigo wao wa deni.

Ugawaji huu wa SDR utaruhusu nchi wanachama kupambana na janga la COVID-19, kuongeza kampeni zao za chanjo na hatua zingine za dharura, mkurugenzi wa IMF amesema katika taarifa.

"Ugawaji mpya wa SDR utanufaisha nchi zote wanachama na kusaidia kuondokana na mgogoro huu wa kiafya," Kristalina Georgieva ameongeza. "Pia itakuwa ishara kubwa ya maamuzi ya wanachama wa IMF kufanya chochote kinachowezekana ili kukabiliana na mdororo mbaya wa uchumi tangu mdororo wa miaka ya 1930."

Ugawaji huu mpya wa SDRs utakuwa wa kwanza tangu ule wa kiasi cha dola bilioni 250 zilizoidhinishwa mnamo mwaka 2009, wakati wa mgogoro wa kifedha.

Ikiidhinishwa, akiba ya nyongeza, ambayo inaweza kubadilishwa kuwa sarafu ya kigeni na nchi wanachama au kugawanywa na nchi masikini, itapatikana baadaye mwaka huu.