DUNIA-WHO--AFYA

Coronavirus: WHO yalaani kukosekana kwa usawa wa chanjo

Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Afya Ulimwenguni (WHO) Tedros Adhanom Ghebreyesus akizungumza wakati wa Mkutano wa Afya Ulimwenguni (WHA) katikati mwa janga la ugonjwa wa Corona (COVID-19) huko Geneva, Uswisi, Mei 24, 2021.
Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Afya Ulimwenguni (WHO) Tedros Adhanom Ghebreyesus akizungumza wakati wa Mkutano wa Afya Ulimwenguni (WHA) katikati mwa janga la ugonjwa wa Corona (COVID-19) huko Geneva, Uswisi, Mei 24, 2021. via REUTERS - CHRISTOPHER BLACK/WHO

Janga la COVID-19 linachochewa na "ukosefu wa usawa" katika usambazaji wa chanjo, mkuu wa Shirika la Afya Dunia (WHO) amesema Jumatatu hii, akiweka malengo mapya ya kulinda raia wa nchi masikini zaidi.

Matangazo ya kibiashara

Zaidi ya 75% ya chanjo zote zimetolewa katika nchi 10 tu, Mkurugenzi Mkuu wa WHO Tedros Adhanom Ghebreyesus amesema wakati wa ufunguzi wa mkutano wa kila mwaka wa mawaziri wa afya wa nchi wanachama 194 wa shirika hilo.

"Hakuna njia ya kidiplomasia ya kusema, kundi dogo la nchi ambazo zinatengeneza na kununua chanjo nyingi duniani zinadhibiti hatima ya ulimwengu wote," amesema.

Hakuna nchi inayopaswa kufikiria "kutoa maneno yasiyoeleweka", bila kujali kiwango chake cha chanjo, maadamu virusi vya SARS-COV-2 na aina zake zinaendelea kusambaa katika nchi zingine duniani, amebaini.

"Ulimwengu unabaki katika hali ya hatari sana," ameongeza.

"Hadi sasa, visa vingi vimeripotiwa tangu kuanza kwa mwaka huu kuliko mwaka 2020. Ikiwa hali ya sasa itaendelea, idadi ya vifo itazidi jumla ya mwaka jana katika wiki tatu zijazo. Inasikitisha sana," Tedros Adhanom Ghebreyesus amesema .

Mpango wa Covax, ukiongozwa na WHO na Muungano wa Chanjo (GAVI), umetoa dozi milioni 72 za chanjo kwa nchi 125 tangu mwezi Februari, kiwango ambacho kinatosha kwa 1% ya raia, amesema.

Pia amehimiza nchi kutoa dozi ya chanjo kwa mpango wa Covax ili kuwezesha 10% ya raia katika nchi zote wawe wamepewa chanjo ifikapo mwezi Septemba na 30% ifikapo mwisho wa mwaka, ikimaanisha kuwa watu zaidi ya milioni 250 watahitaji kupatiwa chanjo katika kipindi cha miezi minne tu.

"Hii ni muhimu kutokomeza ugonjwa huo na vifo, kuhakikisha usalama wa wafanyikazi wetu wa huduma za afya, kufungua tena makampuni yetu na chumi zetu," Mkurugenzi Mkuu wa WHO amebaini.