Uganda - Siasa

Bobi Wine awaambia wafuasi wake kuandamana baada ya kuondoa kesi Mahakamani

Kiongozi wa upinzani nchini Uganda Robert Kyagulanyi maarufu kwa jina la Bobi Wine,
Kiongozi wa upinzani nchini Uganda Robert Kyagulanyi maarufu kwa jina la Bobi Wine, AP - Nicholas Bamulanzeki

Aliyekuwa mgombea urais nchini Uganda Robert Kyagulanyi kwa jina maarufu la  Bobi Wine ametoa wito  kwa wafuasi wake kuazisha  maandamano ya amani kulalamikia kile alichosema ni ushindi wa wizi wa rais Yoweri Museveni baada ya Uchaguzi Mkuu uliofanyika Januari 14 2021.

Matangazo ya kibiashara

Bobi Wine ambaye amedai kushinda uchaguzi huo kwa asilimia 54 amewaambia wafausi wake kuwa wana haki kikatiba kujitokeza kudai ushindi wao.

Wananchi wenzangu amkeni kwa amani bila silaha. Kifungu cha 29 cha katiba yetu kinatupa jukumu la ku ndamana kwa amani kupinga udhalimu wowote. Wanainchi ambao kura zao ziliibiwa muandame, mkienda kwenye Ofisi zote za umaa, kudai majibu, huu ni wito ninaoutoa pia kwa wananchi wetu walio nje ya nchi.

Hatua hii ya mwanasiasa huyo kijana, imekuja wiki moja baada ya kuondoa kesi ya kupinga ushindi wa Museveni katika Mahakama ya Juu kwa kile alichokisema kuwa hakuwa na imani kuwa haki itapatikana.

Tume ya Uchaguzi nchini humo baada ya uchaguzi huo, ulimtanagza rais Museveni ambaye amekuwa madarakani kwa miaka zaidi ya 30 mshindi kwa kupata asilimia 58.38 huku Bobi Wine akiwa wa pili kwa asilimia 35.08.

Jeshi la polisi tayari kupitia msemaji wake  Patrick Onyango limemwonya Bobi Wine na wafuasi wake, kuhusu mpango huo wa maandamano huku maafisa wa usalama wakionekana katika barabara kadhaa za jiji la Kampala.

 Kwa mujibu wa  sheria, wanainchi wana haki ya kuandamana  kwa amani lakini kuna taratibu kadhaa ambazo ni pamoja na kupata ruhusa kutoka kwa  mkuu wa polisi. Lazima watimize hii taratibu. Tunawaonya kwamba hatutawaruhusu kujunja sheria.

 Uganda tangu mwaka 1986 vyombo vya usalama vimehusishwa pakubwa katika siasa za nchi hiyo.