MAHINDI-KENYA-UGANDA-TANZANIA

Kenya yaondoa marufuku ya uingizwaji wa mahindi kutoka Tanzania na Uganda kwa masharti

Mahindi
Mahindi CC0 Pixabay/

Kenya imeondoa marufuku ya uingizwaji wa mahindi kutoka nchi jirani za Tanzania na Uganda, lakini kwa masharti mapya baada ya hatua hiyo kuzua sintofahamu kuhusu hali ya ufanyibiashara chini ya soko la pamoja katika Jumuiya ya Afrika Mashariki.

Matangazo ya kibiashara

Wizara ya Kilimo nchini Kenya, ilichukua hata hiyo wiki iliyopita, kwa kile ilichosema kuwa, mahindi kutoka nchi hizo mbili yalikuwa na kiwango kikubwa cha kemikali aina ya aflatoxin, ambayo ni hatari kwa matumizi ya binadamu na inaweza kusababisha magonjwa kama saratani.

Masharti hayo ni yepi ?

Kenya sasa inataka wadau wote wanaosafirisha mahindi nchini humo, kujiandikisha na Wizara ya Kilimo, na mzigo wa mahindi unaoingia nchini humo lazima uwe na cheti kinachoonesha kuwa kiwango cha aflatoxin hakizidi kile kinachohitajika.

Wafanyibiashara nao sasa watahitajika kutoa taarifa kuhusu eneo yalipo maghala yanayohifadhi mahindi hayo.

Msisitizo wa serikali ya Kenya:

Katibu Mtendaji katika Wizara ya Kilimo Lawrence Angolo amesema hatua ya Kenya ni kulinda usalama wa walaji wa mahindi hayo, na haitarudi nyuma katika juhudi za kulinda usalama wa watu wake.

Aidha, ameongeza kuwa kufahamu yaliko maghala yanayohifadhi mahindi hayo, kutasaidia kuhakikisha kuwa bidhaa hiyo inahifadhiwa katika maeneo salama na sio kukaushwa kwenye barabara za lami.

Tunapojitahidi kuwapa Wakenya chakula salama kwa kuzingatia changamoto tulizonazo za uzalishaji, tunatumai kuwa washirika wetu tunaofanya nao biashara, wataheshimu usalama wa kufanya biashara kwa mujibu wa taratibu za Jumuiya ya Afrika Mashariki, kwa kuzingatia kiwango kinachotakiwa cha aflatoxin.

Masharti haya mapya yanakuja wakati huu wafanyibiashara wakisema hapakuwa na haja ya kuzuia mahindi yote kutoka nchini humo, bali wangechukua hatua kwa yale yaliyoonekana kuwa na sumu.