WHO-TANZANIA-COVID 19

WHO yaitaka Tanzania kutoa takwimu za maambukizi ya Covid 19

Mkurugenzi wa shirika la afya duniani, WHO, Tedros Adhanom Ghebreyesus
Mkurugenzi wa shirika la afya duniani, WHO, Tedros Adhanom Ghebreyesus REUTERS/Denis Balibouse

Shirika la afya  duniani WHO kwa mara nyingine,  limeitaka Tanzania kuanza kutoa takwimu za maambukizi ya Covid 19, karibu mwaka mmoja baada ya nchi hiyo kuacha kutoa takwimu za maambukizi hayo.

Matangazo ya kibiashara

Wito huu unakuja wakati huu kukiwa na maswali mengi kuhusu hali ya kiafya ya kiongozi wa nchi hiyo John Magufuli ambaye hajaonekana hadharani kwa wiki mbili sasa.

Mkuu wa WHO barani Afrika Daktari Matshidiso Moeti, amesema Shirika hilo lipo tayari kuisaidia Tanzania ili kushinda maambukizi hayo.

Tutafurahi kuanza kupokea takwimu kutoka nchini Tanzania kuhusu  hali ya Covid 19 ili tuwasaidie lakini pia tunahimiza nchi hiyo iungane na mchakato wa kupata chanjo, ili wao kama nchi zingine, wawalinde wananchi wao dhidi ya maambukizi ya virusi.

Mwezi Februari, Mkurugenzi Mkuu wa WHO Tedros Adhanom Ghebreyesus aliitaka Tanzania kuchukua hatua madhubuti dhidi ya Covid 19 baada ya abiria wanaotokea  nchini humo kupatikana na virusi hivyo licha ya kupewa cheti cha kutokuwa na maambukizi hayo.

Rais Magufuli alinukuliwa akisema kuwa, chanjo zinazotolewa duniani haziwezi kuaminika na badala yake akatoa  wito kwa Watanzania, kumwomba Mungu na kujifukiza ili kushinda janga hilo.