Samia aapishwa, awataka Watanzania kuweke tofauti kando

Rais mpya wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan
Rais mpya wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan © Ikulu ya Tanzania

Aliyekuwa makamu wa rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, ameapishwa rasmi kuwa rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, baada ya kifo cha aliyekuwa rais wa nchi hiyo John Pombe Magufuli.

Matangazo ya kibiashara

Rais Magufuli, alifariki Jumatano ya terehe 17 kutokana na maradhi ya moyo, ambayo alikuwa akipatiwa matibabu kwa muda sasa.

Samia Suluhu Hassan, aliapishwa katika ikulu ya nchi hiyo, ambapo pamoja na mambo mengine, alitangaza mtiririko wa ratiba ya mazishi ya Magufuli.

Katika hotuba yake ya kwanza kwa taifa rais Samia Suluhu Hassan, aliwashukuru wananchi kwa utulivu pamoja na chama chake.

Nawashukuru CCM kwa kuwa nami tangu tulipopata msiba, nawashukuru pia viongozi wa vyama vya upinzani kwa wingi wa salamu za rambirambi na kunipa pole tangu nilipotangaza msiba huu mkubwa, huu ni wakati wa kuzika tofauti zetu na kuwa wamoja kama taifa.

Rais Samia, pia alitumia sehemu ya hotuba yake kueleza namna alivyofanya kazi na hayati marehemu Dr Magufuli, ambapo amesema:

Dr Magufuli alikuwa kiongozi asiyechoka kufundisha, amenifundisha mengi, amenilea na kuniandaa vya kutosha, tumepoteza kiongozi shupavu, madhubuti, mzalendo, mpenda maendeleo na mwanamapinduzi ya kweli.

Katika sherehe za kuapishwa kwake zilihidhuriwa na viongozi wa zamani, akiwemo rais wa awamu ya tano, Jakaya Kikwete, rais wa awamu ya pili Alhaji Hassan Mwinyi, pamoja na aliyekuwa rais wa Zanzibar, Abeid Aman Karume.

Hata hivyo katika tukio la hivi leo ni viongozi wachache waliokuwa wamevaa barakoa licha ya tishio la uwepo wa ugonjwa wa Corona nchini Tanzania, ambapo kwa majuma kadhaa taifa hilo lilianza kuchukua tahadhari kujikinga.

Samia Suluhu Hassan, anakuwa rais wa kwanza mwanamke kuongoza Tanzania lakini pia katika nchi wanachama za Jumuiya ya Afrika Mashariki.

Anachukua hatamu ya uongozi kipindi ambacho Tanzania imeendelea kusifiwa na taasisi za kifedha kutokana na kupiga hatua kimaendeleo, licha ya ukosolewaji wa baadhi ya hatua ambazo zimechukuliwa.

Pia anaingia madarakani huku nchi ya Tanzania kama mataifa mengi ulimwenguni, yakiendelea kupigana dhidi ya maambukizi ya virusi vya Corona, ugonjwa ambao umesababisha mamilioni ya raia duniani kufariki.