TANZANIA

Samia Suluhu Hassan kuapishwa kuwa rais wa 6 wa Tanzania

Samia Suluhu Hassan, rais wa kwanza mwanamke kuapishwa leo Ijumaa Tanzania.
Samia Suluhu Hassan, rais wa kwanza mwanamke kuapishwa leo Ijumaa Tanzania. AP

Makamu wa rais Samia Suluhu Hassan mwenye umri wa miaka 60, anatarajiwa kuwa rais mpya wa nchi hiyo kwa kipindi kilichosalia katika muhula wa miaka mitano.

Matangazo ya kibiashara

Ibara ya 37 kifungu cha Katiba nchini humo, kinaeleza kuwa, endapo kiti cha Rais kitakuwa wazi kutokana na rais kufariki dunia, kujiuzulu, kupoteza sifa za uchaguzi au kutomudu kazi zake kutokana na maradhi ya mwili au kushindwa kutekeleza kazi na shughuli za rais, basi Makamu wa rais ataapishwa na atakuwa rais kwa muda uliobaki katika kipindi cha miaka mitano.

Baada ya kuapishwa leo Bi.Samia Suluhu Hassan ambaye amekuwa Makamu wa rais tangu mwaka 2015 anatarajiwa sasa kuwa rais hadi uchaguzi mwingine utakapofanyika mwaka 2025.

Anatarajiwa kuwa  mwanamke wa kwanza kushika nafasi hiyo nchini Tanzania, na rais wa pili kutokea Zanzibar baada ya Ali Hassan Mwinyi aliyeliongoza taifa hilo kwa miaka 10 kutoka mwaka 1985 mpaka 1995.

Samia Suluhu Hassan anajulikana vipi kisiasa Tanzania?

Alianza kupata umaarufu wa kisiasa nchini Tanzania wakati alipohudumu kama Makamu Mwenyekiti wa Bunge la Katiba lililoteuliwa mwaka 2014, kuangazia mageuzi ya Katiba nchini humo.

Msomi huyo wa masuala ya Utawala kutoka chuo Kikuu cha Manchester nchini Uingereza, aliwahi kufanya kazi katika mashirika yasiyokuwa ya kiserikali na mpango wa Shirika la Chakula Duniani (WFP)  huko visiwani Zanzibar.