TANZANIA

Philip Isdor Mpango aidhinishwa kuwa makamu wa rais Tanzania

Sehemu ya bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, lililoko mjini Dodoma Tanzania ambako ni makao makuu ya Serikali, ndipo amdidhinishwa Dkt Philip Isdor Mpango, kuwa Makamu wa rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Sehemu ya bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, lililoko mjini Dodoma Tanzania ambako ni makao makuu ya Serikali, ndipo amdidhinishwa Dkt Philip Isdor Mpango, kuwa Makamu wa rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Ikulu/Tanzania

Bunge la Tanzania hii leo limemwidhinisha Dkt Philip Isdor Mpango, kuwa Makamu wa rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa asilimia 100 ya kura zilizopigwa, akichukua nafasi ya Samia Suluhu Hassan ambaye sasa ni rais baada ya kufariki rais John Pombe Magufuli wiki mbili zilizopita.

Matangazo ya kibiashara

Dkt Philip Isdor Mpango ameidhiniswa na Bunge baada ya jina lake kuwasilishwa na rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan ambaye alishauriana na Chama Madarakani, CCM, kupitia Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa kwa mujibu wa Katiba ya nchi hiyo.

Dkt Mpango mtaalam mbobevu wa masuala ya Uchumi amehudumu katika nafasi mbalimbali kwenye serikali Tanzania na hatimaye kuteuliwa kuwa makamu wa rais akiwa katika nafasi ya Waziri wa Fedha na Mipango.

Dkt Mpango amesema kipaumbele chake ni kumsaidia rais Samia ili kuhakikisha Tanzania inaondokana na umasikini na rushwa masuala yanayokwamisha maendeleo ya Watanzania.

Wabunge waelezea hisia zao

Wabunge na mawaziri aliowahi kufanya nao kazi Dkt Mpango hawakuficha hisia zao wakimwelezea kama mtu mwadilifu, mpenda maendeleo na mcha Mungu.

Makamu rais mteule wa Tanzania Dkt. Mpango ataapishwa na jaji mkuu kesho Ikulu ya Chamwino jijini Dodoma saa tisa alasiri na kitakachokua kikisubiriwa ni mabadiliko ndani ya Baraza la Mawaziri ikiwemo nafasi ya Waziri wa Fedha na Mipango iliyoachwa wazi na Dkt Mpango.