KENYA-COVID 19

Kenya yalegeza masharti ya kupambana na Corona, nchi yafunguliwa

Rais wa Kenya Uhuru Kenyatta
Rais wa Kenya Uhuru Kenyatta AP

Rais wa Kenya Uhuru Kenyatta , ametangaza kulegeza masharti ya kupambana na janga la Corona yaliyokuwa yametangazwa mwezi Machi baada ya kuongezeka kwa maambukizi ya virusi hivyo.

Matangazo ya kibiashara

Jiji Kuu Nairobi na Kaunti zingine nne za Kajiado, Machakos, Kiambu na Nakuru zilizokuwa zimefungwa, sasa zimefunguliwa na watu wanaweza kusafiri nchi nzima.

Maeneo ya kuabudu, Makanisa na Misikiti  yamefunguliwa tena katika kauti hizo tano na wanafunzi watarejea Shuleni tarehe 10 Mei  kama ilivyopangwa.

Muda  wa mwisho wa watu kutembea umeongezwa kutoka saa mbili usiku mpaka saa nne usiku, huku watu wakitarajiwa kutembea tena saa 10 Alfajiri.  

Maeneo ya burudani yamefunguliwa tena lakini yatafungwa saa moja jioni.

Hata hivyo, Rais Kenyatta ameonya kuwa serikali haitasita kuchukua hatua zaidi iwapo maambukizi yataongezeka baada ya kuondoa masharti hayo.

Hakuna anayefurahia  hali hii tunayopitia lakini nirudie kusema kuwa iwapo hatutaweza kuacha ubinafasi wetu na  kulinda maisha ya watu na uchumi, basi hatutakuwa na budi kufanya kile ambacho tunastahili kufanya kwa mujibu wa Katiba ili kulinda maisha ya Wakenya.

Kenya imeripoti visa 160,000 na vifo vya watu zaidi ya 2700, huku mwezi Aprili pekee watu zaidi ya  570 walipoteza maisha, na kuwa mwezi ulioshuhudia maafa makubwa tangu kuzuka kwa maambukizi hayo mwezi Machi mwaka 2020.