KENYA-TANZANIA

Tanzania na Kenya zakubaliana kuimarisha biashara na kukuza uhusiano wao

Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan akihutubia kikao cha pamoja cha Wabunge wa Kenya na Maseneta huko Nairobi, Kenya, Mei 5, 2021.
Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan akihutubia kikao cha pamoja cha Wabunge wa Kenya na Maseneta huko Nairobi, Kenya, Mei 5, 2021. REUTERS - MONICAH MWANGI

Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan, ametamatisha ziara yake ya siku mbili nchini Kenya kwa kuwahotubia wabunge na Maseneta jijini Nairobi.

Matangazo ya kibiashara

Katika hotuba yake rais Samia, ameelezea uhusiano wa kihistoria wa nchi yake na Kenya na kueleza kuwa alikuja nchini Kenya kuthibitisha uhusiano huo.

Rais Samia amekuwa rais wa pili wa Tanzania kulihotubia bunge la Kenya baada ya rais mstaafu Jakaya Kikwete kufanya hivyo mwaka 2015.

Wabunge wa Kenya na Maseneta wakifuata hotuba ya Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan katika Majengo ya Bunge huko Nairobi, Kenya, Mei 5, 2021.
Wabunge wa Kenya na Maseneta wakifuata hotuba ya Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan katika Majengo ya Bunge huko Nairobi, Kenya, Mei 5, 2021. REUTERS - MONICAH MWANGI

Kenyatta na Samia wakutana na wafanyabiashara

Viongozi wa Kenya na Tanzania katika kikao chao na wafanyibiashara wa nchi hizo mbili jijini Nairobi, wametoa hakikisho la kuimarisha mazingira ya kufanya biashara kati ya nchi hizo mbili.

Rais Uhuru Kenyatta wa Kenya, amewaambia wawekezaji kutoka nchini Tanzania kuja nchini Kenya na kuwekeza kwa wingi.

Naye rais Samia Suluhu Hassan amewahakikishia wafanyiabishara wa Kenya kuwa, serikali yake imedhamiria kuondoa vikwazo vyote vya kufanya biashara.

Kenya na Tanzania ni washirika wa karibu kwenye biashara kwa miaka mingi lakini kumekuwa na ushindani na vikwazo ambavyo vimeelezwa kutatiza mahusiano hayo ya kibiashara.

Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan amekuwa ziarani ya siku mbili nchini Kenya kuimarisha mahusiano kati ya nchi yake na Kenya.