TANZANIA-AFYA

Ripoti : Tanzania kukumbwa na mlipuko wa tatu ikiwa hatua hazitachukuliwa

Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan, akikagua vikosi vya ulinzi vya Kenya katika Ikulu ya Nairobi, Kenya, Mei 4, 2021.
Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan, akikagua vikosi vya ulinzi vya Kenya katika Ikulu ya Nairobi, Kenya, Mei 4, 2021. REUTERS - BAZ RATNER

Kamati maalum ya wanasayansi iliyoundwa na rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan kutoa thathmini kuhusu hali ya ugonjwa Corona nchini humo, imeonya kuwa nchi hiyo ipo katika hatari ya kukabiliwa na wimbi la tatu iwapo hatua hazitochukuliwa.

Matangazo ya kibiashara

Ripoti ya Kamati hiyo, imetaka serikali nchini humo kuanza kuchukua hatua za kudhibiti kusambaa kwa ugonjwa huo, kuanza kutanagaza watu walioambukizwa virusi vya corona, na kuagiza chanjo.

Kamati hiyo imeishauri serikali kupitia vyombo vyake kulishughulikia suala la chanjo kwa kujiunga na mpango wa covax ulio chini ya mwamvuli wa Gavi.

Mpango wa covax unalenga kuhakikisha nchi masikini kote duniani zinapata mgao sawa wa chanjo licha ya ufinyu wa uwezo wao wa kiuchumi. Mwamvuli wa Gavi unaundwa na mashirika mbalimbali ikiwemo Shirika la Afya Duniani na baadhi ya serikali za nchi tajiri duniani.

Mara ya mwisho kwa Tanzania kutoa takwimu za watu walioambukizwa virusi vya corona ilikuwa mwezi Aprili mwaka 2020 wakati wa utawala wa aliyekuwa kiongozi wa nchi hiyo Marehemu John Magufuli.