UGANDA-AFYA

Uganda yachukuwa hatua kali kukabiliana na ongezeko la visa vya maambukizi

Rais wa Uganda Yoweri Kaguta Museveni.
Rais wa Uganda Yoweri Kaguta Museveni. via REUTERS - PRESIDENTIAL PRESS SERVICE

Shule zimefungwa nchini Uganda, baada ya rais Yoweri Museveni kutangaza hatua hiyo kufuatia ongezeko la maambukizi ya Corona nchini humo. Mikutano ya hadhara imepigwa marufu sawa na safari kutoka Wilaya moja kwenda nyingine, kama njia mojawapo ya kudhibiti maambukizi hayo.

Matangazo ya kibiashara

Masharti haya mapya yaliyotangazwa na rais Museveni Jumapili usiku, yanaanza kutekelezwa kwa siku 42 zijazo.

Museveni ameeleza kuwa hatua hizi zinahitajika ili kudhibiti maambukizi makubwa ya virusi vya corona nchini humo baada ya maambukizi zaidi ya watu 8000 kuripotiwa wiki mbili zilizopita, ikiwa ndio idadi kubwa kuwahi kuripotiwa tangu kuanza kwa janga hilo nchini humo.

Wauzaji wa barakoa na vifaa vingine vya kujilinda na COVID-19 huko Kampala Aprili 2020 (picha ya kumbukumbu).
Wauzaji wa barakoa na vifaa vingine vya kujilinda na COVID-19 huko Kampala Aprili 2020 (picha ya kumbukumbu). © SUMY SADURNI/AFP

Aidha, ameonya kuwa hatua zaidi zitachukuliwa iwapo masharti yaliyotangazwa hayatazingatiwa.

Hata kabla ya tangazo hili la rais Museveni, maafisa wa usalama walikuwa wameanza kuwakamata watu wanaokiuka masharti ya kupambana na janga hilo, na wiki moja iliyopita, watu zaidi ya 2000 walikamatwa kwa kukiuka masharti ya kutembea nje kwa muda usiohitajika.