TANZANIA SIASA

Rais wa Tanzania Samia Suluhu awafutakazi Mkuu wa Wilaya ya Morogoro na mkurugenzi

Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan
Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan © blog.ikulu.go.tz

Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan amewafuta kazi mkuu wa Wilaya ya Morogoro na mkurugenzi wa halmashauri hiyo baada ya kuchukizwa jinsi walivyoshughulikia suala la wafanyabiashara wadogo (Machinga) wilayani humo.

Matangazo ya kibiashara

Wakati akihutubia kwenye mkutano wake na vijana uliofanyika mkoani Mwanza, Juni 15, Rais Samia amemwagiza Waziri wa Tamisemi, Ummy Mwalimu  ambae naye alikuwepo kwenye mkutano huo kutekeleza agizo lake la kutengua uteuzi wa viongozi hao.

"

Kutokana na kutengewa eneo lililo nje lisilofikiwa na wateja, wamachinga Morogoro waliamua kurejea mjini na mamlaka ikaingilia kati kuwaondoa. Sijafurahia jinsi walivyotendewa na DC na mkurugenzi hawana kazi."

"Kwa sababu kuna njia nzuri zaidi ambayo ingetumika kushughulikia hilo..., sio ile iliyotumika. Sijafurahishwa nakuagiza Waziri wa Tamisemi shughulikia hilo," amesema Samia.

Hata hivyo majina ya viongozi hao waliofutwa kazi hayakutajwa lakini mkuu wa Wilaya ya Morogoro ni Bakari Msulwa na mkurugenzi ni Sheila Lukuba.

Viongozi hao wanakuwa wa kwanza kupoteza nafasi zao kwa kutoshughulikia vyema suala la wa machinga tangu Rais Samia alipoingia madarakani Machi 19, 2021.

Mkutano huo ulikuwa ni wa kwanza kuendeshwa na kiongozi huyo tangu aingie madarakani, ambapo amewahimiza vijana kuwa wajitokeze katika mstari wa mbele kulipa ushuru ili kustawisha uchumi wa taifa hilo.

Rais wa Suluhu, amesema kuwa tatizo kubwa katika taifa lake ni ukosefu wa ajira. Aidha amesema serikali yake imejaribu kutatua tatizo hilo kupitia sekta ya utalii, Uchimbaji madini, umeme, ujenzi na elimu huku akidokeza kuwa nafasi za ualimu 6660 zimetangazwa lakini  zaidi ya vijana elfu 20 wametuma maombi hali inayoleta ushindani mkubwa na ishara za ukosefu wa ajira.

Katika hotuba yake rais Samia ametoa wito kwa vijana kwamba licha ya matangazo ya nafsi za kazi katika serikali, kuna wale ambao watanufaika katika nafasi hizo lakini kuna wale ambao hawatapata nafasi za kazi.

"Takwimu nchini Tanzania zinaonyesha kuwa idadi ya vijana ni takriban milioni 20  ajira katika sekta ya umma inaambatana na ukuaji wa uchumi na pia uwezo wa serikali wa kulipa mishahara".

Kufuatia ujenzi wa barabara na vilevile uchimbaji wa bomba la mafuta kutoka Hoima kwenda Tanga, rais Samia amewahimiza vijana kujitokeza kusaka ajira katika mradi huu. Aidha rais ameziomba sekta binafsi kuwekeza katika viwanda ili ziweze kutoa ajira kwa vijana.

Rais Samia amesema kuwa serikali yake imejaribu kuimarisha sekta ya Sanaa na utamaduni kwa kuimarisha haki miliki ambapo kuanzia mwezi Disema wasanii wataanza kupokea mirabaha kutoka kwa vyombo vya habari vinavyopeperusha kazi zao.

Ili kutambua vipaji na kuvikuza mashinani, rais amemwagiza waziri wa michezo kutegeneza viwanja vya michezo katika mikoa ya Tanzania.