BURUNDI-SIASA

Kada wa chama cha CNL atoweka baada ya kukamatwa na jeshi

Wanajeshi wa Burundi wakiwa katika moja ya mitaa ya Bujumbura (picha ya kumbukumbu).
Wanajeshi wa Burundi wakiwa katika moja ya mitaa ya Bujumbura (picha ya kumbukumbu). REUTERS/Goran Tomasevic

Chama kikuu cha upinzani nchini Burundi, CNL cha Agathon Rwasa, kimelazimika kupaza sauti baada ya mmoja wa makada wake kutekwa nyara Ijumaa ya wiki iliyopita, Julai 9, mchana kweupe na mbele ya mashahidi.

Matangazo ya kibiashara

Élie Ngomirakiza, mkuu wa chama hicho katika wilaya ya Mutimbuzi katika mkoa wa Bujumbura alikamatwa na wanajeshi wakiwa kwenye gari la kijeshi lililotambuliwa na mashahidi, chama hicho kinabaini.

Ilikuwa karibu saa 10 mchana kweupe, Élie Ngomirakiza, mkuu wa chama cha CNL katika wilaya ya Mutimbuzi, kaskazini magharibi mwa Bujumbura, alikuwa aanapeleka matofali kwa mteja wake. Alipowasili kwenye lango la mji mkuu wa kiuchumi wa Burundi, Bujumbura, lori lake lilisimamishwa na gari la jeshi.

“Kulingana na habari tuliyonayo leo, kulikuwa na askari kwenye gari. Pia nambari za usajili wa gari hilo zinajulikana ni A031, msemaji wa chama cha CNL, Thérence Manirambona, amesema, huku akiongeza kuwa gari hilo ni la afisa wa jeshi.

Mashahidi waliokuwepo wakati wa tukio hilo wanadai kuwa waliweza kuwatambuwa baadhi ya watu waliokuemo katika gari hilo aina ya 4X4 ya jeshi la Burundi, ambaye ni Luteni-Kanali Aaron Ndayishimiye - anayeongoza kikosi cha 212 kinachopiga kambi katika msitu wa Rukoko, karibu na mpaka na DRC - na maafisa wawili wa utawala katika eneo hilo, ambao walimuonyeshea kidole kada huyo wa chama cha CNL kwa askari ambao "walimteka nyara".

CNL yataka uchunguzi kufanyika

Chama cha CNL kimeomba uchunguzi ili kubaini mazingira halisi ya kutoweka kwake. Kufikia sasa hakuna taasisi ambayo imethibitisha au kukanusha madai ya chama hicho, iwe utawala, polisi, jeshi au hata Tume ya kitaifa ya haki za binadamu (CNIDH).

“Ofisi zetu zinaendelea kuharibiwa. Hii inaonyesha kuwa hakuna uvumilivu wa kisiasa. Tunaomba vitendo hivi vya unyama visikomeshwe ”,amesema Thérence Manirambona.

Angalau wafuasi 30 wa chama cha CNL wamekamatwa na wengine saba wametoweka katika wiki tatu zilizopita pekee, kulingana na chama hicho. Afisa mmoja mwandamizi wa serikali ya Burundi amesema tuhuma "hazina msingi".