RWANDA

Rwanda yachukuwa hatua zaidi kudhibiti Corona

Kwa wakati huu nchini Rwanda kuna asilimia 60 za maambukizi mapya aina ya Delta.
Kwa wakati huu nchini Rwanda kuna asilimia 60 za maambukizi mapya aina ya Delta. © AFP/SIMON WOHLFAHRT

Serikali ya Rwanda imeweka Jiji la Kigali na wilaya 8 kwenye makataa ya kutotoka nje kutokana na maambukizi mapya ya Covid -19 kuanzia siku ya Jumamosi kwa siku 10, huku wanafunzi wakiwa waathirika wakubwa.

Matangazo ya kibiashara

Wanafunzi wa Shule za msingi nchini Rwanda ni miongoni mwa waliothirika kutokana na janga la covid 19.

"Kama munavyojua kwa muda mrefu shule zilikuwa zimefungwa, baada ya kufunguliwa programu zilizokuwa zimeandaliwa kufundishwa kwa muda wa mwaka mmoja zilitumiwa kwa muda wa miaka takriban miwili, amesema Mulindankiko Jean Claude" , Mwalimu mkuu wa shule ya msingi ya SOS Kacyiru, huku akiongeza “ilibidi kuanza upya ili watoto waanze tena masomo yao”.

Shule zote zimefungwa nchini Rwanda ikiwa ni pamoja na vyuo vikuu. Maazimio kuhusu wanafunzi watakaofanya mitihani ya serikali mwezi huu wa julai na Agosti 2021, yatatolewa na wizara ya elimu.

Imepangwa kuwa makataa hayo yataanza rasmi Jumamosi tarehe 17 mwezi huu hadi 26 julai 2021 katika jiji la Kigali na Wilaya 8 ikiwa ni pamoja na Burera, Gicumbi, Kamonyi, Musanze, Nyagatare, Rubavu, Rwamagana na Rutsiro.

Hayo ni baadhi ya maazimio ya Baraza la mawaziri lililokutana jana jumatano kutokana na ongezeko la virusi vya Corona.

Kwa wakati huu nchini Rwanda kuna asilimia 60 za maambukizi mapya aina ya Delta.