TANZANIA-SIASA

Chama cha Chadema chataka Freeman Mbowe kuachiliwa au kufunguliwa mashitaka

Kiongozi wa chama kikuu cha upinzani nchini Tanzania, Freeman Mbowe anayepunga mkono.
Kiongozi wa chama kikuu cha upinzani nchini Tanzania, Freeman Mbowe anayepunga mkono. RFI Kiswahli

Chama kikuu cha upinzani nchini Tanzania Chadema, kupitia Mkurugenzi wake wa mawasiliano na itifaki ya mambo ya nje, kimesema kitafanya kila liwezekanalo kuhakikisha kiongozi wake Freeman Mbowe anaachiliwa au anafunguliwa mashitaka.

Matangazo ya kibiashara

Jumatanu wiki hii chama hicho kimesema kitakwenda mahakamani leo Alhamisi kushinikiza kiongozi wake Freeman Mbowe aachiliwe au ashitakiwe.

Freeman Mbowe ameripotiwa kukamatwa na polisi yeye na wanachama wengine 10 wa chama hicho mjini Mwanza na kupelekwa kusikojulikana wakati walipokuwa wakijiandaa kushiriki kwenye kongamano la kushinikiza kupatikana kwa katiba mpya.

John Mrema amesema Polisi hawakuripoti kumkamata Bw Mbowe, ila walisema kuwa wanawashikilia watu 11 na wa kumi na mbili Mbowe hawakumtaja.

Ripoti zinasema kuwa, Mbowe alikamatwa hotelini mwake usiku wa manane kuamkia siku ya Jumatano.

Kukamatwa kwa Mbowe, kunajiri baada ya kuingia madarakani kwa rais Samia Suluhu Hassan mwezi Machi, kufuatia kifo cha mtangulizi wake John Magufuli na katika kipindi kifupi ambacho amekuwa madarakani ameonekana kubadilisha namna anavyoongoza nchi, lakini chama cha CHADEMA kinasema kukamatwa kwa kiongopzi wao ni ishara kuwa, anaendeleza utawala wa mtangulizi wake.

Mwanzoni mwa wiki hii kiongozi wa Chadema Freeman Mbowe alifanya mkutano na waandishi wa habari ambapo alilalamikia kukamatwa kwa wafuasi wa chama hicho na polisi, pamoja na suala la mabadiliko ya katiba.