TANZANIA-COVID 19

Tanzania yazuia mikusanyiko isiyo ya lazima kupambana na Covid 19

Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan
Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan - AFP/File

Serikali ya Tanzania imesema itaanza kutoa chanjo za kupambana na maambukizi ya virusi vya Covid 19 nchini humo, hivi karibuni, huu ukiwa ni mwelekeo mpya wa serikali ya rais Samia Suluhu Hassan.

Matangazo ya kibiashara

Waziri wa afya nchini humo Dorothy Gwajima ametoa tangazo hilo na kuongeza kuwa serikali inapiga marufuku mikusanyiko ya watu isiyo ya lazima, kuzuia kusambaa kwa maambukizi hayo.

Hata hivyo, Waziri huyo amesema chanjo hizo zitatolewa bure kwa wote wanaohitaji lakini hajasema zoezi hilo litaanza lini.

Waziri Gwajima anasema hali sio nzuri katika kipindi hiki ambacho wagonjwa zaidi ya 600 wakilazwa katika hospitali mbalimbali na wengine zaidi ya 20 wakipoteza maisha kwa mujibu wa takwimu za Julai 21.

Wakati hayo yakijiri, Hospitali ya Rufaa ya  eneo la Kanda ya Kaskazini, KCMC imezidiwa na idadi ya wagonjwa wanaohitaji hewa ya Oksijeni.

Mkurugenzi Mtendaji Hospitali hiyo, Profesa Gilleard Masenga  amesema hospitali hiyo kuzalisha mitungi 400  kwa siku lakini kwa sasa mgonjwa mmoja anatumia mitungi 8 hadi 10 kwa siku.

Tangu mwezi Machi, alipoingia madarakani rais Samia amechukua msimamo tofauti na mtangulizi wake, John Magufuli na kukiri kuwa nchi hiyo ina maambukizi ya Corona.

Mapema mwezi huu, rais Samia alisema hakuna cha kuficha kuhusu maambukizi ya corona nchini Tanzania na kueleza kuwa nchi hiyo ina wagonjwa na inashuhudia mlipuko wa tatu wa janga hili.

Kituo cha kudhibiti magonjwa cha Umoja wza Afrika CDC siku ya Alhamisi limisema, Tanzania, Eritrea na Burundi ndio mataifa pekee ya Afrika ambayo hajaanza kutoa chanjo kwa raia wake.