UGANDA-SIASA

Euro 48,000 kwa kila mbunge kununua gari, zazua mkanganyiko Uganda

Wabunge wa Uganda wakiwa katika kikao huko Kampala.
Wabunge wa Uganda wakiwa katika kikao huko Kampala. REUTERS/James Akena

Wabunge 529 wa bunge la Uganda wiki hii walipokea shilingi milioni 200 za Uganda kila mmoja, au takriban euro 48,000 kwa kila mtu, kwa kitita cha jumla ya euro milioni 25.

Matangazo ya kibiashara

Fedha hizi zimetolewa kwa minajili ya kununuwa magari kwa viongozi waliochaguliwa. Taarifa hiyo imepokelewa shingo upande na raia wa nchi hiyo ambayo imeathiriwa vibaya na mgogoro wa kiafya unaosababishwa na janga la COVID-19.

Msemaji wa serikali Ofwono Opondo ametetea uamuzi huo, akisisitiza kwamba wabunge wana "haki ya kusafiri" kwa kutumia kipando, akitoa mfano wa "mila ya zamani".

Uamuzi haukupokelewa vema na wananchi wote. Sarah Bireete, mwanaharakati wa haki za binadamu, anashutumu hatua hii iliyochukuliwa katikati ya janga la Covid-19 ambalo limeathiri sana nchi hiyo na ambalo linaendelea kusambaa katika maeneo mbalimbali ya nchi.

"Kipaumbele kinapaswa kuwa chanjo kwa raia, kufanya vipimo  ili kujuwa walioambukizwa virusi hivyo na kuhudumia wagonjwa wa Covid ... Lakini tunapoona uamuzi uliochukuliwa na serikali kununulia magari wabunge, wakati hatuna pesa za kutosha kwa chanjo na hospitali hazina dawa muhimu na oksijeni, tunaona kwamba vipaumbele vya nchi vimebadilishwa. Watu wasiojali maisha ya watu, lakini maslahi yao" , amesema mwanaharakati huyo.

Ameongza kuwa: "Mawaziri tayari wana magari mawili kila mmoja, na dereva na huku wakipewa mafuta kwa matumizi ya magari hayo ambayo yanalipwa na wananchi kupitia kodi wanazotozwa. Unaona kuwa wananchi ndio wanaendelea kuumizwa. "

Hasira ziliibuka katika vyombo vya habari na kwenye mitandao ya kijamii. Mnamo mwaka 2018, hatua kama hiyo pia ilisababisha ilizua mvutano. Waandamanaji walivamia hata makao makuu ya Bunge. Lakini kulingana na Joseph Ochieno, mwanasiasa na mchanganuzi wa siasa za Uganda, maandamano haya hayatabadilisha chochote.