RWANDA-HAKI

Rwanda yakaribisha hatua ya Uholanzi kumrejesha nyumbani Venant Rutunga

Picha za waathiriwa wa mauaji ya kimbari nchini Rwanda katika eneo la ukumbusho la mauaji ya Kimbari huko Kigali.
Picha za waathiriwa wa mauaji ya kimbari nchini Rwanda katika eneo la ukumbusho la mauaji ya Kimbari huko Kigali. REUTERS/Noor Khamis

Manusura wa mauaji ya kimbari nchini Rwanda yaliyotokea mwaka 1994, wamepokea kwa furaha kurejeshwa nchini humo kutoka Uholanzi  mmoja wa washukuwa wakuu Venant Rutunga ili kufunguliwa mashtaka.

Matangazo ya kibiashara

Venant Rutunga, mwenye umri wa miaka 72 aliwasili mji mkuu wa Rwanda, Kigali, Jumatatu jioni. Alikabidhiwa kwa maafisa wa Rwanda ambapo anatuhumiwa kuwa alikuwa sehemu ya makada ambao waliandaa mauaji ya Watutsi kusini mwa nchi hiyo.

Mnamo mwaka 1994, Venant Rutunga alikuwa mkurugenzi wa taasisi ya utafiti wa kilimo, Isar Rubona, karibu na mkoa wa Butare. Mauaji yalipoanza, zaidi ya wakaazi elfu moja walikimbilia katika majengo ya taasisi hiyo. Venant Rutunga anashukiwa kuleta askari na wanamgambo wa Interahamwe. Egide Nkuranga, kiongozi wa mpito wa Ibuka, shirika lisilo la kiserikali la Ufaransa linalojikita kuhusiana na kumbukumbu ya mauaji ya Watutsi nchini Rwanda, anasema hakuna shaka: Venant Rutunga alikuwa na jukumu kubwa katika utekelezaji wa mauaji ya kimbari katika sehemu hii ya nchi.

“Alikuwa miongoni mwa viongozi wa Isar. Alikuwa na nafasi kubwa, ya kutekeleza kile anacho kitaka sehemu hiyo ya nchi. Alikuwa mmoja wa watu waliokuwa wakifuatilia utekelezaji wa mauaji ya kimbari yaliyopangwa. Kwa hivyo, alikuwa kiongozi wa operesheni za mauaji ya kimbari ambayo yalikuwa yakitokea nch Rwanda. "

Mnamo mwaka 2000, Venant Rutunga aliomba hadhi ya ukimbizi nchini Uholanzi, lakini alikataliwa, kwa sababu ya kile anachotuhumiwa nchini Rwanda. Karibu miongo miwili baadaye, mwezi Machi 2019, kutokana na matokeo ya ushirikiano kati ya vyombo vya sheria vya Rwanda na Uholanzi, Venant Rutunga alikamatwa katika kijiji karibu na Utrecht.

Baada ya kumaliza rufaa zake zote ili kuepuka kurudishwa nchini Rwanda kuweza kuhukumiwa, anakuwa raia wa tatu wa Rwanda anayeshukiwa kwa uhalifu wa mauaji ya kimbari kurejeshwa na Uholanzi nchini Rwanda.

Kuhusu mkurugenzi mkuu wa zamani wa Isar Rubona Charles Ndereyehe, anayedaiwa kupanga mauaji ya mwaka 1994 katika eneo hili la Rwanda, alikamatwa pia Uholanzi mwezi Septemba 2020. Rwanda inasubiri kurudishwa kwake.