SUDANI KUSINI

Mgawanyiko wajitokeza katika vikosi vya upinzani Sudan Kusini

Makamu wa rais wa kwanza wa Sudan Kusini, Riek Machar.
Makamu wa rais wa kwanza wa Sudan Kusini, Riek Machar. Akuot Chol AFP/File

Afisa wa juu wa jeshi nchini Sudan Kusini ametangaza kumwondoa Makamu wa rais wa kwanza Riek Machar, kama kiongozi wa jeshi linaloegemea upinzani SPLM-IO.

Matangazo ya kibiashara

Luteni Jenerali Simon Gatwech Dual ametangaza hatua hiyo na kusema yeye ndiye kiongozi wa jeshi hilo la upinzani kwa kumtuhumu Machar kwa kwenda kinyume na maono ya jeshi hilo linaloegemea upinzani.

Hatua hii imekuja baada ya kikao cha Majenerali wa jeshi la upinzani na kwa kauli moja, kuamua kuwa Jenerali Gatwech achukue nafasi ya Makamu wa kwanza wa rais kwenye serikali ya mpito.

Mwezi Juni, Machar aliripotiwa kumwondoa Jenerali Gatwech kama kiongozi wa vikosi vya upinzani.

Hata hivyo, Majenerali wanaomuunga mkono Machar, wametupilia mbali uamuzi wa Jenerali Gatwech na kusema mfumo uliopo hauwezi kutikisika.

Watalaam wa masuala ya Sudan Kusini wanasema mgawanyiko ndani ya vikosi vya upinzani, utarudisha nyuma utekelezwaji wa mkataba wa amani wa mwaka 2018 kati ya Machar na rais Salva Kiir.