Kenya: Uchunguzi wa mauaji ya wanajeshi wa Uingereza wafunguliwa tena
Imechapishwa:
Wengi wanajiuliza ikiwa jeshi la Uingereza limefumbia macho mauaji ya msichana mdogo wa Kenya, kitendo kinachodaiwa kuwa kilitekelezwa na askari mmoja kutoka Uingereza. Swali hilo limeibua hisia kubwa nchini Kenya.
Habari za kutoweka kwa mwanamke huyo zilianza mwaka 2012 lakini mahakama iliamua wiki hii kuanzisha upya uchunguzi huo baada ya askari kadhaa wa Uingereza kudai katika magazeti ya Uingereza kuwa aliyehusika na mauaji hayo ni mwenzao na kwamba jina lake ni siri iliyofichwa, inayojulikana kwa muda mrefu na uongozi wa jeshi la Uingereza.
Wanjiru, 21, alioenekana mara ya mwisho akiingia katika mkahawa wa Lions Court mjini Nanyuki akiandamana na wanajeshi wawili wa Uingereza. Miezi miwili baadaye mwili wake ulipatikana katika shimo la maji taka (septic tank) karibu na chumba ambacho alidaiwa alilala.
Uchunguzi kuhusu kifo chake ulifanywa na ikabainika kuwa Wanjiru ambaye alimwacha mtoto mwenye umri wa miaka mitano, aliuawa. Uchunguzi huo uliendeshwa na mahakama ya Nanyuki. Uingereza ina kituo cha kijeshi katika mji huo.
Hayo yanajiri wakati Waziri wa Ulinzi Eugene Wamalwa, Jumanne aliwahakikishia wabunge kwamba serikali ya Uingereza imejitolea kushirikiana na Kenya katika juhudi za kuhakikisha kuwa mwanajeshi wake aliyemuua Agnes Wanjiru mjini Nanyuki, Kaunti ya Laikipia anaadhibiwa.
Akiongea alipofika mbele ya Kamati ya Bunge kuhusu Ulinzi na Mahusiano ya Kigeni Bw Wamalwa alisema kuwa amepata hakikisho hilo kutoka kwa Waziri wa Ulinzi wa Uingereza Ben Wallace na Balozi wa Uingereza nchini Jane Marriott.
"Ningependa kuwahakikishia kwamba tumefanya mashauriano na serikali ya Uingereza kuhusu suala hili lenye umuhimu wa kitaifa. Leo asubuhi nilikutana na balozi wa Uingereza na mwenzangu wa Uingereza na wamenihakikishia kuwa mwenajeshi huyo ataletwa nchini ili ashtakiwe kwa mujibu wa sheria za nchi hii,” aliambia kikao cha kamati hiyo kilichoongozwa na Mbunge wa Saku Dida Rasso.
Inspekta Jenerali wa Polisi Hillary Mutyambai kwa mara nyingine aliamuru kuwa Idara ya Upelelezi wa Jinai (DCI) ishughulikie kesi hiyo kwa lengo la kuhakikisha kuwa mshukiwa amehukumiwa kwa mujibu wa sheria.