UGANDA-USALAMA

Uganda: Mashambulizi ya kujitoa muhanga, "jambo jipya" linalotia wasiwasi

Magari yaliyoharibiwa na kutelekezwa baada ya milipuko huko Kampala, Uganda Novemba 16, 2021.
Magari yaliyoharibiwa na kutelekezwa baada ya milipuko huko Kampala, Uganda Novemba 16, 2021. AP - Nicholas Bamulanzeki

Wakati mashambulizi ya kujitoa muhanga ya Jumanne, Novemba 16 yalidaiwa na kundi la Islamic State, polisi wa Uganda wananyooshea kidole cha lawama ADF, kundi la waasi linaloendesha harakati zake katika nchi jirani ya DRC.

Matangazo ya kibiashara

Tayari mwishoni mwa mwezi Oktoba, serikali ilihusisha kundi la ADF mashambulizi mawili ya mabomu mjini Kampala. Baadhi ya washukiwa wake walikuwa wamekamatwa. Kwa upande wa mtafiti wa Uganda Frederick Golooba-Mutebi, anasema mashambulizi haya ya kujitoa mhanga ni jambo geni.

Inashangaza kwamba nchini Uganda sasa tuna hali mpya ya milipuko ya kujitoa mhanga. Sio kawaida kwa kweli. Mara ya mwisho ilikuwa miaka kumi iliyopita, wakati wahusika walijilipua katika umati wa watu waliokuwa wakitazama mechi ya soka ya Kombe la Dunia. Lakini kama tulivyoweza kuona kwenye video zilizorekodiwa na kamera za CCTV- watu wakibeba mikoba na kujilipua, hii ni mpya.

Hata kabla ya mashambulizi hayo kudaiwa, polisi wa Uganda waliwalaumu waasi wa ADF. Unafikiria nini ?

Katika taarifa, polisi waliwanyooshea kidole waasi wa ADF (Allied Democratic Forces). Labda ni kweli, lakini labda si kweli. Hatujui. Sikumbuki, ADF hivi majuzi walidai kuhusika na mashambulizi kama haya. Lakini ukweli ni kwamba wakati wowote kunapotokea mashambulizi, polisi wanalaumu ADF. Kwa kukosekana kwa uthibitisho, napendelea kuwa mwangalifu. Sio ADF pekee wanaoweza kuandaa aina hii ya mashambulizi. Inaweza kuwa kundi lingine.

Je, unafikiria kundi gani lingine?

Watu waliolipua mabomu mjini Kampala miaka kumi iliyopita walikuwa walitokea nje ya nchi, nchini Somalia. Uganda ina wanajeshi nchini Somalia wanaopigana dhidi ya kundi la Kiislamu la Al-Shabab; hilo linaweza kuwa jambo linalowezekana. Siku hizi, pia tunasikia kuhusu kundi la Islamic State, ambalo linasemekana kuwa washirika wa ADF. Kama ni ADF, kundi la Islamic State, makundi hayo mawawili kwa pamoja, sijui. Ninachomaanisha ni kwamba hakuna uwezekano mmoja tu. ADF ni moja, Al-Shabab ni nyingine.

Una maoni gani kuhusu mashambulizi haya dhidi ya Bunge na polisi?

Nadhani walio nyuma ya mashambulizi haya wanataka kuonyesha kwamba wana uwezo wa kushambulia vituo muhimu na vinavyolindwa vyema, vituo vinavyohusishwa na huduma za usalama au serikali. Hii ni kutaka kuonyesha kuwa wanaweza kumlenga yeyote wanayemtaka.