Polisi yaendelea kuwasaka washukiwa wa shambulizi la hivi karibuni Kampala
Imechapishwa:
Nchini Uganda, wahubiri wengine wawili wa dini ya Kiislamu wamekamatwa kwa madai ya kuhusishwa na mashambulizi mawili ya bomu yaliyotokea wiki iliyopita jijini Kampala.
Idadi ya watu waliokamatwa na maafisa wa usalama mpaka sasa imefikia 108.
Waliokamatwa ni Sheikh Swaibu Segujja na Sheikh Muhammed Ssemwanga wote kutoka wilaya ya Luwero ambayo iko kilomita 64 kaskazini mwa Kampala.
Kukamatwa na kuuawa kwa washukiwa hasa kutoka dini ya Kiislamu kimeleta malalamiko kutoka uongozi wa Kiislamu nchini Uganda.
Bungeni, upinzani umependekeza mazungumzo ya amani kati ya serikali na kundi la waasi la ADF.
Katika hotuba yake siku ya Jumamosi, rais Yoweri Museveni aliwashauri waasi wa ADF na wale waliohusika na mashambulizi ya Bomu kujisalimisha au wafuatiliwe ndani na nje ya Uganda.