Uganda-Burundi

Uganda yaendelea kusaka manusura, Rais wa Burundi aachia wafungwa

Reuters / Alessandro Di Meo

Serikali ya Uganda inaendelea na juhudi za kusaka manusura wa maporomoko ya Udongo ambayo yalichangiwa na mvua zinazonyesha nchini humo na kusababisha vifo vya watu wanaotajwa kufikia zaidi ya mia moja.

Matangazo ya kibiashara

Waziri wa Maafa nchini Uganda Stephene Malinga amesema wamepeleka mitambo mikubwa ambayo itasaidia kufukua udongo ambao umewafukia wananchi hao baada ya kutokea kwa maporomoko.

Waziri Malinga anasema kwa sasa serikali inapambana kuhakikisha inapata suluhu ya kudumu juu ya maafa ambayo yameendelea kutokea katika eneo la Bududa kila mara na kuchangia vifo.

Katika hatua nyingine Rais wa Burundi Pierre Nkurunziza ametangaza msamaha kwa wafungwa kati ya elfu tatu na elfu nne wa nchi hiyo ambao walikuwa wanatumikia vifungo cha chini ya miaka mitano jela na wale wanaokabiliwa na maradhi.

Rais Nkurunziza ametangaza msamaha huo kwa wafungwa ikiwa ni sehemu ya maandalizi ya kusherehekea miaka hamsini ya uhuru wa nchi hiyo sherehe ambazo zinatarajiwa kufanyika tarehe mosi ya mwezi Julai.

Naibu Msemaji wa Rais Nkurunziza, Willy Nyamitwe amesema Kiongozi huyo ameseini amri ya kutoa msamaha wakati nchi hiyo inajiandaa kusherehekea maika hamsini tangu ipate uhuru wake.