TANZANIA

Madaktari wa Tanzania wataka tume huru kuchunguza unyama aliofanyiwa Dk. Ulimboka

RFI

Jumuiya ya Madaktari nchini Tanzania imetaka uwepo wa Chombo Huru cha kufanya uchunguzi kubaini wale ambao wamehusika kwenye kutekwa, kupigwa na kuumizwa kwa Mwenyekiti wao Dokta Ulimboka Steven.

Matangazo ya kibiashara

Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Madaktari Dokta Edwin Chitage ameonekana kuchukizwa na hatua ya vitisho wanavyoendelea kuzipata lakini pia anaendelea kutilia shaka uhuru wa Tume inayofanya uchunguzi.

Katibu Mkuu wake Nicholaus Mgaya wa Shirikisho la Vyama Vya Wafanyakazi nchini Tanzania, TUCTA amejitokeza kulaani kitendo cha kutekwa kwa Dokta Ulimboka.

Serikali tayari imeteua Tume ya uchunguzi ambayo inajiegemeza kubaini wale ambao wamehusika kwenye utekaji, upigaji na uumizaji wa Mwenyekiti wa Jumuiya ya Madaktari nchini Tanzania Dokta Ulimboka Steven.

Afya ya Mwenyekiti wa Jumuiya ya Madaktari nchini Tanzania Dokta Ulimboka Steven ambaye alitekwa na watu wasiojulikana na kasha kumpiga kabla ya kumtupa katika msitu wa Mabwepande imeanza kuimarika.

Afisa Habari wa Kitengo Cha Mifupa cha Hospitali ya Muhimbili , MOI, Juma Almasi amesema Dokta Ulimboka ambaye anapatiwa matibabu akihudumiwa na jopo la Madaktari anaendelea vyema kama anavyoeleza

Katika hatua nyingine Dokta Ulimboka akizungumza kwa taabu kutokana na maumivu yanayoendelea kumtesa amesema kwa sasa angependa kupata mapumziko badala ya muda mwingi kuutumia kuzungumza na watu.

Nao mgomo wa madaktari umeendelea katika Hospital za Rufaa nchini wakati huu ambapo serikali ikitoa wito wa kuanza kutumia Madaktari wastaafu ili kuokoa jahazi kwa kuwahudia wagonjwa wanaoendelea kutaabika kwa kukosa matibabu.