Kenya

Serikali ya Kenya ipo tayari kuzungumza na kundi la Pwani si Kenya

Reuters/Christian Hartmann

Kufuatia mkutano wa dharura wa viongozi wa masuala ya usalama nchini Kenya kukutana hapo jana kujadili hukumu ya mahakama kuu kuhusu kubatilisha uamuzi wa awali wa kulizuia kundi la MRC, waziri mkuu Raila Odinga amesema serikali iko tayari kuzungumza na viongozi wa kundi hilo.

Matangazo ya kibiashara

Mkutano ulisema utaheshimu uamuzi wa mahakama kuu lakini serikali haitosita kutumia nguvu zaidi kuwadhibiti wafuasi wa kundi hilo ambao wataendelea kutishia usalama wa raia wengine ambao hawawaungi mkono.

Kauli ya waziri mkuu inakuja kufuatia juma hili mahakama kuu ya kenya kubatilisha uamuzi wa serikali uliotangazwa kulipiga marufuku kundi hilo kwa tuhuma za ugaidi, jambo ambalo mahakama imesema serikali haikuwa na ushahidi wa kutosha kudhibitisha maneno yake.

Kundi la MRC limekuwa likinadi sera za Mombasa kujitenga na Kenya kwa kauli mbiu ya Pwani si Kenya.

Kundi hilo baada ya kuhalalishwa limesema litaendelea na harakati za kujitenga kwa Mombasa huku wakiamini kuwa sehemu hiyo ina haki ya kuwa nchi huru kwa sababu mikataba ya kuungana baada Kenya kupata uhuru kutoka kwa mkoloni Mwingereza.

Kundi hilo pia limesema kuwa litakuwa tayari kufanya mazungumzo na Serikali ya Kenya baada ya kundi lao kurasmishwa kwani awali lilijulikana kama kundi haramu likiwa katika harakati za Pwani si Kenya.