UGANDA

Uganda yaadhimisha miaka 50 ya Uhuru, Rais Yoweri Museveni asema nchi imepiga hatua

Reuters/Edward Echwalu

Uganda hii leo inaadhimisha miaka 50 ya uhuru huku nchi hiyo ikijipanga kuongeza kasi ya maendeleo kwa kukuza uchumi wake kutokana na rasilimali mbalimbali zilizopo nchini humo.

Matangazo ya kibiashara

Rais wa Uganda Yoweri Kaguta Museveni amesema kuwa katika kipindi cha zaidi ya miaka 20 nchi yake imepiga hatua kubwa za kimaendeleo.

Amesema kuwa nchi yake hivi sasa inaelekeza nguvu katika kuinua maendeleo ya kiuchumi kwa kuboresha matumizi ya teknolojia, sekta ya kilimo, mafuta na gesi.

Pia amesema kupatikana kwa mafuta na gesi hivi karibuni ni hatua ambayo itasaidia nchi hiyo kuwa na umeme wa kudumu utakaosaidia kuboresha sekta ya uzalishaji nchini humo.

Amesema sekta ya utalii nayo itapewa kipaumbele ili kujipatia pato zaidi la nje kwa ajili ya maendeleo ya kiuchumi.

Hata hivyo upande wa upinzani umesusia sherehe za uhuru wa Uganda kwa madai kuwa serikali ya Rais Yoweri Kaguta Museveni inakabiliwa na vitendo vya ulaji rushwa.