DR Congo

Kundi la waasi wa M23 labadili jina na kujiitia Jeshi la Ukombozi wa Congo

Waasi wa kundi la M23 baada ya kuuteka mji wa Rumangabo Julay mwaka huu
Waasi wa kundi la M23 baada ya kuuteka mji wa Rumangabo Julay mwaka huu REUTERS/James Akena

Kundi la waasi wa M23 wa nchini Jamuhuri ya Kidemokrasia ya Congo, wanaoshutumiwa kuhatarisha usalama wa mashariki mwa nchi hiyo, wamesema kuwa wamebadili jina la jeshi lao na kuwa wanajiandaa kujitetea dhidi ya mashambulizi yaliyopangwa kutekelezwa na Jeshi la Serikali ya nchi hiyo.

Matangazo ya kibiashara

Kiongozi wa M23, Jean-Marie Runiga amewaambia wanahabari kuwa M23 sasa kundi hilo linaitwa Jeshi la Ukombozi wa Congo (Congolese Revolutionary Army (ARC).

Kundi hilo, ambalo limekuwa likishutumiwa na Makundi ya haki za Binaadam kuwa wamekuwa wakijihusisha na vitendo vya ubakaji dhidi ya Wanawake na Wasichana na kutekeleza mauaji kuashiria kisasi dhidi ya Jeshi la Serikali, liliundwa mwezi May na wapiganaji wa zamani, waasi wa jamii ya Tutsi ambao walijiunga na jeshi chini ya makubaliano ya amani ya mwaka 2009, makubaliano ambayo yanadaiwa kutotimizwa kwa asilimia miamoja.

Runiga amelishutumu Jeshi la Congo kushirikiana na vikosi vya FDLR vya Rwanda, vinavyoelezwa kuwa vya waasi vilivyoundwa na jamii ya kabila la Wahutu ambao awali walikuwa Wanajeshi wa Jeshi la Rwanda kabla ya kulazimishwa kuondoka baada ya mauaji ya halaiki ya mwaka 1994.

Hata hivyo Juma lililopita, jeshi la Congo FARDC, lilitowa taarifa ya makundi ya M23 kuungana na kundi hilo la waasi wa Kihutu wa Rwanda, ili kuendesha mashambulizi zaidi.

Umoja wa Mataifa umeshutumu Rwanda na Uganda kuwaunga mkono Waasi, Shutma zilizopingwa na nchi hizo, huku Rwanda ikiinyooshea kidole DRCongo kwa kuunga mkono waasi wa Rwanda wa FDLR waliopiga kambo nchini DRCongo na ambao baadhi yao wanatafutwa na Rwanda wakishutumiwa kuwa na mkono katika mauaji ya Kimbari, ambayo kwayo watu 800,000 waliuawa wengi wao jamii ya waTutsi.