Burundi

Waandishi wa habari Burundi waandamana kutaka Hassan Ruvakuki aachiwe huru

AFP PHOTO/Esdras Ndikumana

Kwa mara ya kwanza nchini Burundi jana waandishi wa habari wameandamana kwenye ofisi za wizara ya sheria wakipinga hatuwa ya mahakama ya hivi karibuni ya kumzuwia jela kwa kipindi cha miaka mitatu mwandishi habari wa Burundi Hassan Ruvakuki.Waandamanaji hao wamesema Ruvakuki ambaye ni mwandishi habari wa Redio Bonesha FM na pia ni ripota wa RFI Kiswahili hana hatia hivyo anatakiwa kuachwa huru.

Matangazo ya kibiashara

Ruvakuki alitiwa mbaroni mwaka jana kwa tuhuma za kwenda nchini Tanzania katika kambi ya waasi kutekeleza kazi yake.

Mahakama ya mwanzo ilimuhukumu kifungo cha maisha jela kwa makosa ya Ugaidi, na baadaye kukata rufaa.

Polisi mjini Bujumbura ilijaribu kuwazuia waandamanaji hao, waliokuwa na lengo pia la kudai sheria ifuate mkondo wake kwa watu wote wanaotiwa jela bila hatia.

Tangu kutolewa kwa hukumu ya rufaa ya Hassan Ruvakuki kumekuwa kukitolewa mashinikizo mbalimbali ili mwandishi huyo wa habari aachiwe huru.

Upande wa wanasheria wa Hassan Ruvakuki ulipanga kuwasilisha rufaa nyingine kupinga hukumu hiyo kwa kuamini kuwa mteja wao hana hatia na kutaka haki itendeke.