KENYA

Kenyatta atamba matokeo ya awali uchaguzi nchini Kenya

Uhuru Kenyatta, mgombea urais wa muungano wa Jubilee
Uhuru Kenyatta, mgombea urais wa muungano wa Jubilee REUTERS/Noor Khamis

Wakati wakenya wakiendelea kusubiri kutangazwa kwa matokeo ya jumla ya uchaguzi mkuu nchini humo mara baada ya zoezi la kupiga kura kukamilika hapo jana,matokeo ya awali ya uchaguzi huo yanaonesha kuwa mgombea urais kwa tiketi ya muungano wa Jubilee, Uhuru Kenyatta anaongoza kwa asilimia 54.60% akifuatiwa na Raila Odinga wa muungano wa Cord mwenye asilimia 40.30% matokeo ambayo hata hivyo yanabadilika kadiri muda unavyozidi kusonga. 

Matangazo ya kibiashara

Usiku kucha matokeo ya uchaguzi huo yameendelea kukusanywa kutoka katika vituo vya kupigia kura huku karibu theluthi ya vituo vya kupigia kura vikituma matokeo majira ya asubuhi leo Jumanne.

Wapiga kura hiyo jana walisimama katika mistari kadhaa yenye umbali wa mamia ya mita wakiendelea kungoja kwa amani nje ya vituo vya kupigia kura kukamilisha zoezi hilo katika uchaguzi unaodaiwa kuwa na utata kuliko chaguzi zilizowahi kutokea nchini Kenya.

Aidha kabla ya zoezi la kupiga kura vurugu za umwagaji damu zilitokea katika eneo la Pwani mjini Mombasa ambapo polisi sita na washambuliaji sita waliuawa katika mashambulizi mawili tofauti, huku mabomu kadhaa yakilipuliwa na kumjeruhi mtu mmoja huko Mandera mpakani na Somalia.