KENYA-MRC

Viongozi wa kundi la MRC mjini Mombasa wanaotaka mjitengo na serikali ya Kenya wanamatumaini ya kuzungumza na serikali mpya

Viongozi wa kundi linalotaka mkoa wa pwani nchini Kenya kujitenga na taifa hilo la Mombasa Republican Council MRC wamesema wana imani na Serikali mpya ya Uhuru Kenyatta kuwa itafanya nao kikao cha kujadili matatizo yanayo wakumba watu kutoka eneo hilo la Pwani ya Kenya.

Viongozi wa kundi la MRC mjini Mombasa
Viongozi wa kundi la MRC mjini Mombasa
Matangazo ya kibiashara

Kundi hilo la MRC lilikuwa likiomba kufanya mkutano na serikali kuzungumzia matatizo yanayo wakabili ya kutaka mkoa huo wa Pwani kujitenga na Kenya na kuwa taifa huru, jambo ambalo lilikuwa likipingwa vikali na viongozi wa serikali iliopita chini ya rais Mwai Kibaki.

Katibu mkuu wa MRC Randu Nzairuwa, ameiambia RFI kuwa wanaimani na uongozi mpya wa rais Uhuru Kenyatta wa kufanya mazungumzo na serikali mpya, baada ya kulia kwa muda mrefu kukaa na serikali kujadili kuhusu dhulma zilizo fanyika zitatatuliwa namna gani, kwakuwa kuna mikataba iliotiwa saini na ambayo imekuwa ikipewa kisogo.

Kundi la MRC limekuwa likidai  mikataba ambayo lina lalamikia ni halali na ilitiwa sahihi na waziri mkuu wa zamani wa Kenya marehemu mzee Jomo Kenyatta ambae ni baba wa rais Uhuru Kenyatta.

Randu Nzairuwa amesema kinacho wapa matumaini ni kwamba mikataba iliotiwa saini wakati wa uhuru ilitiwa saini na baba yake Uhuru rais Jomo Kenyatta, na rais Uhuru Kenyatta anaonekana ni mtu wa mazungumzo hivyo wanamatumaini kuona wanaketi kwenye meza ya mazungumzo kujadili kuhusu mikataba hiyo na sio kuipa kisogo kama ilivyokuwa kwa serikali iliopita.